*Aliambatana na mkewe, mama mzazi kwenda kwa Babu
*Ataka Mchungaji asaidiwe, Jenerali Msuguri naye abugia
*Wazungu waminika, wajanja waanza kuiba teknolojia yake
*Daktari asema imeponya ukimwi, dawa yaisha kwa muda
Na Timu ya Mtanzania, Samunge
WAZIRI Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali David Musuguri ni miongoni mwa malefu ya watu waliofika katika Kijiji cha Samunge, Loliondo mkoani Arusha kupata “Dawa ya Maajabu ya Mungu” kutoka kwa Mchungaji mstaafu, Ambilikile Masapile.
Wakati Jenerali Musuguri alipata dawa juzi jioni, Sumaye, akiwa na mama yake mzazi na mkewe, walipata dawa jana mchana.
Akizungumza na Timu ya Mtanzania katika mahojiano maalumu muda mfupi baada ya kunywa dawa hiyo, Sumaye alisema: “Kwa kweli najisikia furaha, naamini kabisa kwa jinsi nilivyoona mazingira yale, naamini ni dawa ya kweli na itasaidia sana watu.”
Kwa Watanzania wengine, alisema: “Kwa kweli ningelipenda Watanzania wenzangu tujaribu kumsaidia kadri inavyowezekana (Mchungaji) ili aweze kutoa huduma, na watu waendelee, wenye matatizo waweze kufika huku.”
Mvua kubwa zilizonyesha jana katika eneo la Sumange na maeneo jirani yalisababisha mito ifurike, na hivyo kusababisha adha kubwa kwa watu waliofika kupata dawa.
Sumaye na msafara wake ni miongoni mwa walioonja adha hiyo kwa msafara wake kukwama kwenye udongo wenye utelezi. Alidumu katika hali hiyo kwa dakika kadhaa kabla ya kuendelea na safari yake ya kurejea mkoani Manyara.
Kwa upande wake, Jenerali Musuguri ambaye alitoka kijijini kwake Butiama, alisema baada ya kunywa dawa hiyo amejisikia mwenye furaha na siha njema tofauti kabisa na alivyofika Samunge.
Alisema mabega yalikuwa yakimuuna, lakini jana asubuhi aliweza kuamka na kutosikia maumivu yoyote.
Pia alisema sukari yake ilikuwa ikipanda hadi 39, lakini alipopima jana asubuhi alikuta imeshuka kwa kiwango ambacho hajapata kukiona.
Akionekana kujawa na furaha, alishuka ndani ya gari lake wakati msafara wake ulipokuwa umekwama kutokana na foleni kubwa ya mamia kwa mamia ya magari.
“Najisikia furaha sana, sina maumivu tena, sukari ilikuwa ikipanda hadi nakaribia kufa, lakini kwa kweli leo nimeshangaa kuona sukari imeshuka sana, haya ni maajabu,” alisema Jenerali huyo.
Kadhalika, viongozi mbalimbali waliendelea kumiminika Samunge kupata dawa, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Monica Mbega, naye alionekana akiwa nyuma, mbali kabisa kwenye msafara kwenda nyumbani kwa Mchungaji Masapile.
Kama ilivyotarajiwa, watu wa rangi na dini tofauti waliendelea kumiminika Samunge, hali ambayo imekuwa ikiwastaajabisha watu wengi.
Kwa upande wake, Daktari wa Tiba ya Magonjwa ya Macho Wilaya za Ngorongoro na Simanjiro, Dk. Richard ole Nkambi, ametoa ushuhuda wa namna dawa hiyo ilivyoweza kuwatibu watu wenye magonjwa mbalimbali.
Alisema awali baada ya kupata taarifa hizo walipatwa na mshituko na baadaye walianza kufanya utafiti wa kina kubaini ukweli.
“Timu yetu ya madaktari tulijiridhisha baada ya kubaini kwamba matibabu haya yalikuwa yanahusisha zaidi pia imani,” alisema Dk. Richard.
Hata hivyo alipoulizwa na Mtanzania kama anao ushahidi wowote wa mgongwa wa ukimwi aliyekunywa dawa hiyo na kupata nafuu alisema kwamba: “Nina ushahidi wa mtu ambaye alikuwa na ukimwi na mume wake alifariki na yeye alikuwa akiendelea kutumia dawa za ARV.
“Lakini baada ya kunywa dawa hii hivi sasa huyo mtu kwa ushuhuda wangu anaendelea vizuri na tayari amekwenda kupima kwenye Hospitali ya Wasso na amekutwa hana maambukizi, huu ni ushahidi ambao mimi ninao,” alisema Dk. Richard.
Akitoa ushuhuda kwa upande wake alisema kwamba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa miaka mingi na mara mwisho alifanyiwa vipimo nchini Ujerumani.
Hata hivyo baada ya kutumia dawa hiyo hivi sasa amekuwa akiendelea vizuri kwani sukari iliyokuwa ikimsumbua haipo tena mwilini mwake.
Alisema Hospitali ya Taifa Muhimbili wamechukua sampuli ya dawa hiyo na kubaini kuwa ina uwezo wa kutibu magonjwa sugu mengi. Kwa mujibu wa maelezo yake, Muhimbili na Taasisis nyingine za kiafya wanaendelea na utafiti zaidi wa dawa hiyo.
Mchungaji apewa Usalama wa Taifa wamlinde
Mchungaji Masapile ameimarishiwa ulinzi kwa kupewa vijana wa Usalama wa Taifa.
Jana walinzi hao walionekana wakiwa makini kuhakikisha kuwa wanakabiliana na njama zozote za kumdhuru.
Pamoja na Usalama wa Taifa, wapo askari polisi waliopiga kambi katika Kijiji cha Samunge na kwenye eneo la utoaji dawa. Moja ya dhima waliyonayo ni kuhakikisha ulinzi kwa Mchungaji huyo unakuwa imara na wa uhakika.
Mchungaji asema watu wa mataifa wanakuja
Mchungaji huyo amesema kuwa Mungu amempa maono kuwa mataifa yote ya ulimwengu yatakwenda kwake kupata tiba.
Mchungaji huyo alitoa tamko hilo jana kijijini hapo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya mapumziko ya chakula cha mchana.
“Ni kweli ndivyo ilivyo, Mungu amenipa maono kwamba mataifa yote watakuja hapa wanaosumbuliwa na magonjwa niliyoyataja kwamba watakuja kutumia dawa hapa na wala si pengine.
“Sasa nina mambo ambayo nataka kuwaambia wenzetu wanaokuja hapa hasa wale wanaowaleta wagonjwa mahututi hapa. Hii si hospitali ya rufaa, watu wanakuja kabla hawajatufikia sisi wengine wanapoteza maisha ndani ya magari.
“Wengine wanakuja na dripu kitu ambacho sisi hatuna, nimejaribu kuongea hata na madaktari wengine ambao wanakuja hapa, lakini wananiambia hawawezi kumzuia mtu ambaye anataka kumchukua mgonjwa wake, lakini nimekataa hilo wasifanye hivyo.
“Serikali ijaribu kuzuia jambo hilo si jambo jema. Jingine ambalo nataka kulizungumzia na mnisaidie kuwaeleza watu, kuna watu ambao wameanza kuwaambia vijana wa huku kwetu ambao wanajua miti hiyo tunayoitumia kwamba wawachimbie, na wapo ambao wameshachimbiwa tayari kwa lengo la kwenda kutengeneza dawa.
“Sasa nawambia ya kwamba si kweli, huo ni wizi sikubali mtu yoyote mahali popote kupewa dawa na mtu kwamba mimi nimeitambua dawa hiyo. Mungu hakuagiza hivyo, naomba Taifa letu lijaribu kuwatangazia mataifa mengine kuwa dawa ya aina hiyo haitakuwa dawa, hadi pale Mungu atakapoagiza vinginevyo.
“Kwa wakati huu amemruhusu mtu mmoja tu ambaye ni mimi kutoa dawa hii… nitakapochimba dawa hiyo na mwingine akachimba, Mungu ameniambia kwa huyo mtu si dawa, kwa hiyo watu wasidanganywe na matapeli.
“Kuhusu masharti ya dawa hakuna, ila mimi nimeweka sharti moja, si Mungu, nawaambia watu kwamba ukitumia dawa hii basi kama wewe ni mtumiaji wa pombe usinywe siku uliyokunywa dawa, na kama sharti hili lisingekuwa sawa, basi Mungu angeniambia.”
Hofu yatawala
Watu waliofika kwa Mchungaji Mstaafu Ambilikile Masapile, kupata dawa,
juzi walikumbwa na taharuki na kuonyesha huzuni kubwa baada ya
kuambiwa dawa imemalizika.
Waliambiwa imemalizika kutokana na ukosefu wa kuni za kuchemshia dawa
hiyo, jambo ambalo liliwahuzunisha wengi.
Huduma ilisimama kuanzia saa 10 jioni hadi saa 12 jioni ili kuwezesha
upatikanaji kuni na uchemshaji dawa nyingine.
Mamia ya watu walionyesha huzuni kubwa, wengine wakishika tama na
kuonekana kukata tamaa.
Hali hiyo haikuweza kumalizwa na wasaidizi wa Mchungaji huyo ambao
mara zote walisema dawa ipo, lakini tatizo lilikuwa kuni.
Kutokana na hali hiyo, Serikali wilayani Ngorongoro ilitoa gari kwa ajili ya kukusanya kuni kutoka porini.
Baadaye huduma hiyo iliendelea, lakini kabla ya hapo Mchungaji Masapile aliwaomba radhi watu waliokuwa na shauku ya kupewa dawa hiyo.
“Tunategemea vyombo vya watu kama vina kazi nyingine huwezi kumlazimisha akupe gari lake usombe kuni, taratibu tuendelee kuomba.
“Kilichotukwamisha hapa sasa hivi ni kuni ndiyo maama tumesimama kwa muda huu, mtuwie radhi, hatuna jeuri, hatuna majivuno kwenye kazi ya Mungu. Ni mambo ambayo yako nje ya uwezo wetu,” alisema.
Mpishi wa dawa hiyo, Barnaba Nangulo (41), alisema wanajitahidi kuchemsha dawa baada ya kupata kuni ili huduma iendelee kama kawaida.
Hata hivyo, baadhi ya watu wamekuwa wakiirushia lawama Serikali Kuu kwa kupuuza kabisa kuweka miundombinu na vifaa katika Kijiji cha Samunge ili kuhudumia maelfu kwa maelfu ya watu wanaokwenda kutibiwa.
Wanailaumu Serikali kwa kupuuza kuweka mahema makubwa ili kuwakinga
watu dhidi ya mvua na jua. Jana mvua kubwa ilinyesha na kukwamisha kwa
muda utoaji huduma ya dawa.
Tatizo jingine ambalo limeonekana kijijini hapa baada ua mvua kunyesha ni maeneo ya kujihifadhi na mvua, hata hivyo wakati watu wakiendelea kuhaha kujihifadhi kutokana na mvua kwa upande wa watu
wenye magari wamejikuta wakiwa na wakati mgumu wa kupishana kutokana
na ufinyu wa barabara.
Pia Serikali haijaonyesha nia ya dhati ya kujenga vyoo katika eneo hilo, hali inayosababisha kutapakaa kwa vinyesi.
Pamoja na tatizo hilo bado changamoto ya uchafuzi wa mazingira imeendelea kushamiri kutokana na chupa za maji, makasha ya vitu mbalimbali kuzagaa kijijini hapo.
Taarifa hii imeandikwa na Manyerere Jackton, Masyaga Matinyi na Eliya Mbonea waliopo Samunge, Loliondo
Habari kwa hisani ya New Habari