Sumatra wajipanga kuwajibu matrafiki

Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Israel Sekirasa

Na Joachim Mushi

SAKATA la malalamiko yaliyotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) dhidi ya baadhi ya askari polisi rafiki kuwa ndio wamiliki wa magari mabovu na yasiofuata taratibu katika sekta ya usafirishaji abiria, limeingia sura mpya baada ya SUMATRA kudai wanajipanga kutoa tamko.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Meneja Mawasiliano wa SUMATRA, David Mziray alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii kuhusiana na kauli ya Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani kutaka SUMATRA kuwataja askari wanaovunja sheria za usafirishaji ili washughulikiwe.

Mziray katika maelezo yake alisema hawezi kuendeleza malumbano juu ya suala hilo na kinachofanyika sasa ni wao kukaa, kujadiliana na kuangalia kama kuna sababu ya kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo.

“Hatuwezi kuendeleza majibizano kupitia magazeti, sisi tutakaa na kupitia hoja zilizotolewa na kuangalia namna ya kufanya…kama kuna sababu tutatoa ufafanuzi,” alisema Mziray.

Machi 23, mwaka huu Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Israel Sekirasa, aliwashitaki polisi kwa Rais Jakaya Kikwete, kwamba ndiyo chanzo cha uvunjaji wa kanuni, sheria na taratibu za usafiri barabarani kutokana na baadhi yao kumiliki daladala nyingi na ambazo ni mbovu.

Hata hivyo siku moja baada ya kutoa kauli hiyo, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, katika vyombo vya habari alimtaka Sekirasa kutoa ushirikiano polisi ili wazifanyie kazi tuhuma alizozitoa.

Mpinga alisema Jeshi hilo halijafurahishwa na kitendo cha Sekirasa kutoa tuhuma hizo mbele ya Rais Kikwete, kwani angeweza kuwasilisha malalamiko hayo kwao kwa lengo la kufanyiwa kazi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda Mpinga, alisema kauli aliyoitoa Sekirasa kwao haina tofauti na kuwachongea kwa Rais Kikwete jambo ambalo halileti picha nzuri.

“Hatupingi kauli aliyoitoa, isipokuwa katika hali ya kawaida, kwanza alipaswa kutuwasilishia malalamiko hayo ili tuyashughulikie, hasa ikizingatiwa kuwa sisi sote ni wasimamizi wa sheria hizo,” alinukuliwa Kamanda Mpinga na vyombo vya habari.

Mwisho.