Sudani Kusini Kujadiliwa EAC Oktoba

Sudani Kusini Kujadiliwa EAC Oktoba

Sudani Kusini Kujadiliwa EAC Oktoba

Na Ronald Ndungi, EANA, Arusha

MAJADILIANO juu ya ombi la Sudani Kusini kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yameahirishwa hadi Oktoba mwaka huu, Mkutano wa wakuu wa nchi EAC ulisema Jumatano. Mwenyekiti wa Mkutano huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema mjini hapa kwamba kucheleweshwa huko kutatoa nafasi kwa Sudani Kusini kufanya maandalizi ya kitaifa na mashauriano.
 
“Hata hivyo EAC imeshafanya maandalizi ya utaratibu na mpango wa majadiliano na Jamhuri ya Sudani Kusini juu ya nchi hiyo kuingizwa katika jumuiya,” Kenyatta alisema wakati wa kikao Maalumu cha 12 cha wakuu wa EAC. Alisema kuwa mgogoro uliozuka Sudani Kusini mwaka jana, bado unaendelea katika baadhi ya maeneo nchini humo.
 
“Hayo yanatokea licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini na pande zinazohusika katika mgogoro huo mapema mwaka huu,” alisema Kenyatta.
 
Kiongozi huyo wa Kenya alisema EAC inatoa wito madhubuti kwa pande zinazopigana kuheshimu hadidu za rejea za makubaliano ya amani yaliyofikiwa, linaripoti Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA).

Wakati huohuo Baraza la Mawaziri la EAC juzi lilisema kwamba asilimia 57.9 ya maamuzi na maelekezo ya wakuu wa nchi wanachama yemetekelezwa mpaka sasa. Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC, Phyllis Kandie alikiambia kikao Maalumu cha 12 cha Wakuu wa Nchi za EAC kwamba jumla ya maamuzi na maelekezo 121 yametekelezwa wakati wa vikao vya kawaida na vikao maalum vya EAC tangu mwaka 2001.
 
“Hata hivyo, asilimia 42 ya maamuzi yakiwakilisha asilimia 34.7 yameshughulikiwa kinusunusu wakati mengine 9 au asilimia 7.4 yakiwa bado hayajaguswa kabisa,” alisema Kandie.
 
Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa EAC, Rais Kenyatta alitoa wito kwa nchi wanachama pamoja na Sekretarieti ya Jumuiya hiyo kutekeleza haraka mambo ambayo bado hayajakamilishwa.