Na Mwandishi Wetu
TAIFA la Sudan Kusini limetoa ufafanuzi juu ya hatua yake ya kusitisha uzalishaji mafuta na mpango wa nchi hiyo wa kusafirisha shehena hiyo ya mafuta kwenda nje ya nchi kupitia Bandari za Kenya.
Ufafanuzi huo umetolewa jana mjini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Fedha wa Sudan, Dk. Marial Awou Yol katika mkutano wa tathmini ya usimamizi wa rasilimali za mafuta kwa nchi za Afrika. Waziri huyo amesema nchi hiyo imefikia hatua hiyo kutokana na tofauti kati ya nchi yake na Taifa la Sudan Kaskazini.
Dk. Awou Yol amesema tangu nchi hiyo itangazwe kuwa taifa huru Julai mwaka 2011, kumekuwa na tofauti za kimaslahi kati yake na Sudan Kaskazini na kwamba usafirishaji wa mafuta kupitia bandari ya Lamu nchini Kenya ni sehemu ya mipango ya muda mrefu ya kushughulikia tofauti hizo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi wa Tanzania, Gregory Teu amezitaka nchi za Afrika kujenga mazingira ya uwazi na usimamizi bora wa rasilimali za madini ili ziwe na umuhimu katika uchumi na maendeleo ya nchi husika na raia wake.