KIKOSI CHA TAIFA STARS kimeondoka leo alfajiri kwenda Windhoek, Namibia kwa ajili ya mechi ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya wenyeji itakayochezwa Machi 5 mwaka huu.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ina msafara wa watu 25 unaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Timu imefikia hoteli ya Safari jijini humo.
Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Sam Nujoma, na kikosi cha Taifa Stars kipo chini ya Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi ambaye ana leseni A ya ukocha inayotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Namibia (Brave Warriors) inayofundishwa na kocha Ricardo Mannetti imeingia kambini jana (Machi 2 mwaka huu) kwa ajili ya mechi hiyo ambayo tiketi zake zilianza kuuzwa Februari 28 mwaka huu.
MECHI YA YANGA, AHLY YAINGIZA MIL 488
Mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly kutoka Misri iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki imeingiza sh. 448,414,000.
Mapato hayo yametokana na watazamaji 50,202 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 7,000, sh. 13,000, sh. 25,000 na sh. 35,000. Yanga ilishinda mechi hiyo kwa bao 1-0.
Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 68,402,135.59, gharama za kuchapa tiketi ni sh. 10,343,219, waamuzi na kamishna sh. 14,665,930 na matangazo sh. 15,679,000.
Uwanja sh. 50,898,557.31, gharama za mchezo sh. 33,932,371.54, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)/Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 33,932,371.54 wakati Yanga ilipata mgawo wa sh. 220,560,415.01.
Nayo mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa jana (Machi 2 mwaka huu) imeingiza sh. 20,610,000 ambapo kila klabu ilipata mgawo wa sh. 4,402,492 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 3,143,898.31.
MECHI YA MLALE, LIPULI YARUDISHWA NYUMA
Mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Mlale JKT na Lipuli iliyokuwa ichezwe Machi 9 mwaka huu Uwanja wa Majimaji mjini Songea sasa itachezwa Machi 5 mwaka huu.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefanya mabadiliko hayo ili kuipunguzia gharama timu ya Lipuli ya Iringa ambayo jana (Machi 2 mwaka huu) ilicheza mechi mjini Songea dhidi ya Majimaji.