Stars yajipanga kuikabili Gambia

Stars yajipanga kuikabili Gambia

KIKOSI cha Taifa Stars ambacho jana kilicheza na Ivory Coast hapa Abidjan na kupoteza kwa mabao 2-0 kinaendelea kujinoa kwa mechi ijayo dhidi ya Gambia itakayochezwa Jumapili ya Juni 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa programu ya Kocha Kim Poulsen, Taifa Stars imefanya mazoezi leo asubuhi kwenye uwanja wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ivory Coast (FIF) ambao uko pembezoni mwa jiji la Abidjan.

Timu hiyo itafanya tena mazoezi Juni 4 mwaka huu asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani saa 1.30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo itawasili Dar es Salaam, Juni 5 mwaka huu saa 1.40 asubuhi.

Kocha Kim ambaye amekuja na wachezaji wote hapa ukiondoa wanne ambao ni majeruhi (Thomas Ulimwengu, Nurdin Bakari, Haruna Moshi na Nassoro Masoud Cholo) amesema hivi sasa wameelekeza akili yao kwenye mechi ijayo dhidi ya Gambia.

“Safari ya kujenga timu ndiyo imeanza. Mechi dhidi ya Ivory Coast imepita na ninawashukuru wachezaji kwa kucheza kwa mujibu wa maelekezo na kujituma. Mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa yaliyosababisha tuwape Ivory Coast mabao mepesi.

“Lakini kama nilivyosema mechi hiyo imepita, hivi sasa tunaangalia mechi ijayo dhidi ya Gambia. Hatuna muda mwingine wa kujipanga na ndio maana niliamua kuja na wachezaji wote Abidjan,” amesema Kim.

Mechi dhidi ya Gambia itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Gambia ilitoka sare ya bao 1-1 na Morocco katika mechi iliyochezwa juzi jijini Banjul.

Hata hivyo, Taifa Stars haitakuwa na nahodha wake msaidizi Aggrey Morris ambaye alionesha kadi nyekundu dakika ya 65 baada ya kupata ya pili ya njano kwenye mechi dhidi ya Ivory Coast iliyochezwa Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny jijini Abidjan.