STARS Kushiriki Michuano ya COSAFA

Ngasa

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imethibitisha kushiriki michuano ya kombe la COSAFA nchini Afrika Kusini kufuatia mwaliko wa Baraza la vyama vya soka Kusini mwa Afrika (COSAFA).

Michuano ya kombe la COSAFA inatrajiwa kuanza kutimua vumbi katikati ya mwezi Mei mwaka huu nchini Afrika Kusini, na ratiba ya hatua ya awali ya makundi inatarajiwa kutangazwa leo jioni saa 1:00 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki moja kwa moja na kituo cha Luninga cha Supersport 4.

Taifa Stars itakuwa juu (seeded) katika hatua ya makundi, ambapo nchi nane zitagawanya katika makundi mawili na washindi wa kila kundi wataingia hatua ya robo fainali, nchi nyingine zitakazoanzia kwenye makundi ni Lesotho, Madagascar, Marutius, Namibia, Seychelles, Swaziland.

Katika kila kundi, timu zote zitacheza michezo mitatu na mshindi wa kila kundi ataingia katika hatua inayofuata ya robo fainali itakayozijumuisha nchi za Afrika Kusini, Botswana, Ghana, Malawi, Msumbuji na Zambia ambazo zimeingia katika hatua ya pili kutokana na nafasi zao kwenye msimamo wa viwango vya FIFA.

Kombe la COSAFA lilianza mwaka 1997 linajumuishaa nchi 16 wanchama kutoka Kusini mwa Bara la Afrika, limekua likifanyika kwa kushirikisha nchi wanachama waliopo Kusini mwa bara la Afrika.

Nchi wanachama wa COSAFA ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Comoros, Lesotho, Madagascar, Malawi, Maurtius, Mayotte, Msumbuji,Namibia, Reunion, Sychelles, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.

SALAMU ZA RAMBIRAMBI.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini – TFF amepeleka salamu za rambirambi kwa familia ya Bw. Nyama, kufuatia kifo cha mwamuzi mstaafu Mohamed Nyama ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya waamuzi ya TFF kilichotokea jana kwao Nachingwea- Lindi.

Marehemu Mohamed Nyama wakati wa uhai wake alikuwa mwamuzi wa daraja la kwanza ambaye pia alitambuliwa na FIFA, Nyama anatarajiwa kuzikwa leo jioni kwao Nachingwea mkoani Lindi na TFF itawakilishwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Bw. Athumani Kambi.

Katika salam zake kwa familia ya Nyama, kwa niaba ya TFF, familia ya mpira wa miguu na watanzania Rais Malinzi amewapa pole wapenzi wa mpira wa miguu nchini katika kipindi hiki kigumu cha maombelezo.

KILA LA KHERI AZAM, YANGA, KMKM NA POLISI

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF), limezitakia kila la kheri na ushindi timu za Azam na Young Africans katika michezo yao ya marudiano itakayofanyika mwishoni mwa wiki hii .

Azam FC itakuwa ugenini siku ya jumamosi mjini Khartoum, Sudan kucheza mchezo wa marudiano na wenyeji timu ya El Merreikh ambapo katika mchezo wa awali uliofanyika Chamazi jijini Dar es salaam Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Jijini Gaborone nchini Botswana katika kombe la Shirikisho, timu ya Young Africans watacheza na wenyeji timu ya jeshi ya BDF XI siku ya ijumaa katika mchezo wa marudiano pia, ambapo katika mechi ya awali Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mjini Zanzibar KMKM wataikaribisha timu ya AL Hilal ya Sudan siku ya jumamosi katika Uwanja wa Aman, huku kikosi hicho Maalum cha Kuzuia Magendo kikihitaji ushindi wa kuanzia mabao 3-0 ili kuweza kusonga mbele, kufuatia kupoteza mchezo wa kwanza Khartoum kwa mabao 2-0.

Timu ya Polisi Zanzibar itakuwa mwenyeji wa timu ya FC Mounana kutoka nchini Gabon siku ya jumapili katika mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika,ikihitaji ushindi wa mabao 5-0 ili kufuzu hatua inayofuata baada ya kupoteza mchezo wa awali kwa mabao 4-0.

Kwa niaba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, famili ya mpira na watanzania wote wanawatakia kila la kheri na ushindi katika michezo hiyo ya marudiano ambapo timu hizo zitakua zikipeperusha bendera ya Taifa.