Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limesaini makubaliano ya awali (MoU) na Shirika la Madini la Korea (KORES)kwa ajili ya shughuli za utafiti, uchimbaji na uuzaji wa madini nchini.
Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya utiaji saini huo Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Ramadhani Khatibu amesema kuwa makubaliano hayo yanalenga ushirikiano baina ya nchi ya Tanzania kupitia shirika lake la STAMICO na shirika la KORES katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uuzaji wa madini nchini.
Khatib amesema makubaliano hayo yatalenga mradi wa madini aina ya manganese wa Kabulwanyele uliopo Mpanda huko Katavi ambapo eneo la mradi huo linamilikiwa na shirika la STAMICO.
Akizungumzia mchango wa shirika la STAMICO katika mradi huo Hatibu amesema kuwa shirika la KORES litachangia gharama za utafiti ikiwa ni pamoja na wataalamu na wakati shirika la STAMICO litachangia kwa kutoa wataalamu pamoja na vifaa vya utafiti.
Khatib aliongeza kuwa, shughuli za awali za mradi huo zinatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya maandalizi ya awali kukamilika
Wakati huo huo Rais wa Shirika la Madini la KORES Shin- Jong Kim amesema kuwa ana uhakika kuwa mradi huu utakuwa na manufaa kwa nchi ya Tanzania na nchi ya Korea kwa ujumla kwani kutakuwa na mpango wa kubalilishana uzoefu.
“ Mfano tutakuwa tunaleta wataalamu kutoka Korea kuja kushirikiana na wataalamu wa hapa Tanzania kwa ajili ya kubalishana ujuzi na uzoefu hali kadhalika wa Tanzania kwenda Korea kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.’’ Alisisitiza Jong Kim.
Jong Kim aliongeza kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na nchi ya Tanzania ili kukuza sekta ya madini na kuleta maendeleo ya kiuchumi zaidi
Akizungumzia faida ya nchi itakayopata baada ya kuanza kushirikiana na nchi ya KORES, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Gray Mwakalukwa alisema kuwa mradi huo unatarajia kuongeza idadi ya ajira kwa wataalamu wa Tanzania.
Aliongeza kuwa teknolojia katika utafiti na uchimbaji wa madini itaongezeka kutokana na kuwepo kwa progamu ya kubalishana uzoefu na vifaa vitaongezwa vya kisasa.