Na Anna Nkinda – Maelezo
KUTOFAHAMU stadi za maisha kumewafanya watoto wengi wa kike kushindwa kumaliza masomo yao kwa kijiingiza katika vishawishi mbalimbali na hivyo kutotimiza ndoto zao za maisha. Hayo yamesemwa jana na Anita Masaki ambaye ni Afisa Mradi wa TUSEME kutoka Ulingo wa Wanawake waelimishaji wa Afrika (FAWE) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uwezeshaji wa jinsia kwa wanafunzi wa kike wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo Rufiji mkoani Pwani.
Masaki alisema watoto wa kike wanakutana na changamoto mbalimbali za maisha hii ikiwa ni pamoja na kutendewa matendo maovu lakini wanaogopa kusema ila kama wakiwa wamefundishwa stadi za maisha ni rahisi kwao kuweza kukabiliana nazo.
“Malengo ya TUSEME ni kuwawezesha wasichana ili waweze kuchambua matatizo yanayowafanya wawe nyuma kitaaluma, kupaza sauti na kujieleza kwa uhuru juu ya matatizo yao na kushirikiana na viongozi kutatua matatizo yanayowakabili ili kuinua kiwango cha taaluma,” alisema Masaki.
Ofisa Mradi huyo aliendelea kusema katika mila na desturi za kiafrika mwanamke anaonekana ni mtu wa daraja la pili wakati umefika sasa wa kuvunja mila na desturi zinazomkandamiza mtoto wa kike kwani wengi wao wanakosewa lakini wanaambiwa wasiseme. Masaki alisema,“Vunjeni ukimya kwani baada ya mafunzo haya mtakuwa mmepata mbinu za kuzungumza na kupata stadi za maisha na hivyo kuweza kusoma vizuri”.
Mtatumia sanaa za maonyesho kufikisha ujumbe kwa jamii yenu kwa kutenga siku moja au mbili kwa kila muhula wa masomo na kuweza kuongea na walimu wenu kwa kuwatajia changamoto zinazowakabili.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kutoka Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Dk. Mikidadi Alawi alisema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kujitambua kwani wanafunzi wengi wa kike wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za mimba za utotoni na utoro. Dk. Alawi alisema wakati wa mafunzo hayo wanafunzi wataweza kujadili changamoto wanazokabiliana nazo kwani wengi wanakutana na matatizo ambayo yanawafanya wakatize masomo yao kwa kuwa wameshindwa kusema.
“Watoto wa kike wakiweza kujitambua kwa kupata stadi za maisha na kujua jinsi ya kuishi katika jamii itawafanya kuwa majasiri na kuweza kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao,” alisema Dk. Alawi.
Naye Makamu Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Obeth Mwakatobe aliwataka wanafunzi hao kuwa makini na wasikivu kwa kuyashika yale watakayofundishwa na baada ya hapo wabadilike na kuwa walimu wa watoto wenzao kwa kuwafundisha stadi za maisha. Mwalimu Mwakatobe pia aliwasihi wanafunzi hao kusema changamoto zinazowakabili ili waweze kusikika na hivyo kutatuliwa matatizo yao.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamedhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na Taasisi ya WAMA ambayo ndiyo wamiliki wa shule hiyo yenye wanafunzi 363 wa kidato cha kwanza hadi cha tano.