SPIKA WA BUNGE AMPA SIKU TANO MBUNGE WA ARUSHA MJINI, KUTOA UTHIBITISHO WA KAULI YAKE


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Mungano Mheshimiwa Anne Makinda amempa muda wa siku tano Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini Mhe. Godbless Lema kutoa uthibitisho wake bungeni kuhusiana na kauli aliyoitoa kuwa Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda amelidanganya Bunge.
Spika Makinda ametoa uamuzi huo kutokana na kanuni za Kudumu za Bunge ibara ya 63 (6) inayomtaka mbunge ambaye hakuridhika na maelezo yaliyotolewa na Mbunge mwenzake bungeni kutoa uthibitisho huo kwa kiwango cha kuliridhisha bunge, papo hapo au katika muda atakaopewa na Spika kwa ajili ya kufanya hivyo.
“Mhe Lema nakupa mud ahadi tarehe 14 Februari, 2011 katika kikao cha asubuhi ulete uthibitisho wako kuhusu tuhuma zako,” alisema Mhe. Makinda. hatua hiyo imefikiwa baada ya Waziri Pinda kulieleza bunge wakati akijibu maswali ya papo kwa papo kuwa, “utaratibu uliofuatwa kumpata meya wa jiji la Arusha ulikuwa sahihi.
Meya ni halali na naibu wake ni halali.”baada ya maelezo hayo, Mhe Lema alisimama na kuomba Mwongozo wa Spika kuwa, “Mhe Spika naomba Mwongozo wako iwapo Kiongozi mkubwa anaweza kusimama hapa na kulidanganya bunge, kanuni zinasemaje? “kanuni ya 63 (8) inampa mamlaka Spika kumwadhibu kwa kumsimamisha mbunge huyo asihudhurie vikao vya bunge visivyozidi vitano.
Maelezo ya Waziri Mkuu kuhusu uchaguzi wa Meya wa Mji wa Arusha yalitolewa bungeni baada ya Mbunge wa Viti maalum (Manyara) Mhe. Martha Umbulla, kumtaka aeleze ni tatizo gani lililopelekea vurugu hizo, na kuitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya chama cha siasa kilichosababisha vurugu zile.
Mhe Pinda alisema, “Hili ni eneo jingine linalosikitisha sana, Baaraza la madiwni la Halmashauri ya Arusha lilifanya mkutano wake tarehe 17 Desemba, 2010, kwa mujibu wa kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni, wajumbe wote 31 walipata taarifa ya kikao hicho na kuhudhuria.
Kikao hicho kulijumuisha madiwani 16 kutoka chama cha CCM, madiwani 14 kutoka Chadema na diwani mmoja kutoka TLP. “Lakini mkutano ulipoanza zikawepo hoja kuwa Mhe . Mary Chatanda ambaye ni mbunge wa viti maalum wa Tanga na Katibu wa CCM wa mkoa wa Arusha Anaingiaje kwenye mkutano huo? , CCM nao wakasema Mhe Rebeca Mgodo hajaapishwa naye anaingiaje? ” akasema na kuongeza kuwa baada ya kuwasiliana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tamisemi ikaonekana kuwa wote wawili ni wajumbe halali wa mkutano huo.
Kutokana na ubishi huo kuchukua siku nzima na taratibu haziruhusu baada ya saa 12 jioni kuendelea na kikao, wajumbe wakakubaliana kikao hicho kifanyike kesho yake tarehe 18/12/2010 saa 4:30.”muda ulipofika Chadema wakawa wanaingia wanatoka, wakati wajumbe 16 kutoka CCM na Mmoja kutoka TLP wakiwa ndani, kikao kikafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu na mjumbe wa CCM akashinda kiti cha Umeya, nafasi ya Unaibu meya ikaenda kwa mjumbe wa TLP kutokana na wagombea wa Chadema na CCM kutopata kura,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, baada ya kupiga kura Mhe. Lema, akaingia katika ukumbi huo na kudai kuwa ni zamu ya Chadema ndipo polisi walipoitwa na mkutano ukahairishwa. “baada ya hapo tukapata taarifa ya maandamano, tukasema kuna haja gani na kwanini wasiende mahakamani?.
Kwa hesabu za kawaida hata mtoto mdogo wajumbe 16 kwa wajumbe 14 utashindaje?” akasema. hata hivyo Mhe. Pinda amelieleza bunge kuwa hakuna haja ya serikali kuichukulia hatua Chadema kutokana na kusababisha vurugu hizo ila Chadema wana haja ya kujenga chama kinachoaminika kwa wananchi, kwasababu vitendo vya kususia wanavyoendelea kufanya haviwezi kujenga chama kizuri.