Spika Makinda awafunda viongozi wa Bunge

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa Semina Elimishi ya wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge na Kamati ya Uongozi katika hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam. Picha na Magreth Kinabo–MAELEZO

Na Magreth Kinabo–MAELEZO

VIONGOZI wa Bunge wametakiwa kufuata majukumu yao ya kazi, maadili na kufahamu mipaka yake ya kiutendaji ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea.

Kauli hiyo imetolewa leo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda wakati akifungua semina elimishi ya siku mbili ya wajumbe wa Tume ya Utumishiwa Bunge na Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati ya Uongozi wa Bunge inayoendelea katika Hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa Bunge ni mojawapo ya mihimili ya dola na ni chombo muhimu katika uongozi na hatma ya nchi, hivyo umuhimu wa chombo hicho ni sharti uendane na maadili ya viongozi wake.

“Ufanisi wa Taasisi ya Bunge unategemea utendaji kazi wa vyombo viwili kwa sababu vyombo hivi ndiyo washauri wakuu wa Spika katika kuliongoza Bunge,” alisema Spika Makinda.

Baadhi ya washiriki katika Semina Elimishi ya wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge na Kamati ya Uongozi wakiendelea na semina yao.


Aidha aliongeza kuwa Kamati ya Uongozi ndicho chombo chenye mamlaka ya kumshauri Spika kuhusu hoja na masuala mbalimbali ya takayowasilishwa bungeni, ambapo kwa upande wa Tume ya Utumishi wa Bunge ndio kiungo kikuu cha Utawala na Usimamizi wa Huduma mbalimbali zitolewazo kwa wabunge na watumishi wa Bunge.

Spika Makinda aliongeza kuwa vyombo hivyo viwili vinategemeana, hivyo ni muhimu kukutana ili kubadilishana mawazo nauzoefu wanamna ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi. Aliwataja viongozi hao kuwa wazi na huru katika majadiliano ya mada zitakazo wasilishwa.

Spika Makinda alizitaja mada tano ambazo zinatarajiwa kuwasilishwa kwa wajumbe hao kuwa ni pamoja na maadili, uongozi na utawala bora, majukumu ya Tume ya Utumishi wa Bunge na Kamati ya Uongozi na Mahusiano yake, taratibu za kiutendaji na mifumo ya mawasiliano Serikali, nafasi ya mbunge katika uongozi, itifaki na usalama, ikiwemo mahusiano ya mihimili mitatu (Bunge, Utawala na mahakama katika uongozi wa nchi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kilindi, Beatrice Shellukindo akizungumza katika semina hiyo, amesema itawasaidia kuelewa majukumu yapi yanatakiwa kiusahihi kutekelezwa na vyombo hivyo viwili.