Spika Anne Makinda; Sigombei Tena, Awataka Atakao ‘Wa-Miss’

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu tamko la kutogombea nafasi ya Spika msimu huu katika mkutano wake  uliofanyika jijini Dar es salaam.

Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini maelezo anayotoa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda (hayupo pichani) alipotoa tamko la kutogombea tena nafasi hiyo msimu huu.

Na Jacquiline Mrisho-MAELEZO, Dar es Salaam

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda ametangaza rasmi kutogombea nafasi ya Uspika wa Bunge baada ya kuliongoza Bunge la 10 kwa kipindi cha miaka mitano. Makinda ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.

“Kama yalivyo matakwa ya kisheria na demokrasia ya hapa nchini wanasiasa wanatumikia nafasi zao mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitano na kisha wanarudi kuomba tena ridhaa kwa wananchi kuongoza,” alisema Makinda.

Mheshimiwa Makinda aliongeza kuwa anaona wakati umewadia kwa yeye kuwaachia wengine nao washike wadhifa huo katika Mhimili huo muhimu wa kusimamia Serikali. Mbali na hayo Makinda aliendelea kusema kuwa ametumikia nafasi mbalimbali katika Siasa kwa kipindi cha miaka 40 ndani ya Bunge, ikiwemo nafasi ya Waziri, Mwenyekiti wa Bunge, Naibu Spika na Spika hivyo kwa sasa ameamua kung’atuka katika masuala ya uongozi.

Hata hivyo Spika amewaambia waandishi wa habari kuwa katika kipindi cha uongozi wake, Bunge lilifanyakazi kwa ushirikiano na liliweza kuisimamia Serikali hadi kupelekea baadhi ya Mawaziri kujiuzulu. Ameongeza kuwa Bunge la 10 lilifanikiwa kubadilisha mfumo wa bajeti kwa kuweka sheria mpya za bajeti ambayo iliongeza nidhamu katika matumizi ya fedha.

Makinda alisema kuwa atawakumbuka Waheshimiwa mbalimbali katika bunge aliloliongoza akiwemo Tundu Lissu, Halima Mdee, Felix Mkosamali, Moses Machali, John Mnyika na wengine ambao alifanya nao kazi kwa ushirikiano.