WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya soko la Kimataifa la Samaki la Feri, kukutana na makampuni mbalimbali yanayouza gesi ili kupata kampuni inayouza kwa bei nafuu zaidi lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama wakaangaji wa samaki sokoni hapo.
Pia Waziri Mkuu Majaliwa alimtaka Meneja wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi kuhakikisha wanakuwa na kifaa maalumu cha kupimia ujazo wa mitungi ya gesi sokoni hapo ili kubaini kama ni sahihi.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumanne, Machi 22, 2016) wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo ambapo aliridhishwa na unavyofanya kazi.
Waziri Mkuu ambaye ametumia dakika 44 kulitembea soko hilo, alitoa maagizo hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamesema wamekuwa wakiuziwa gesi kwa bei kubwa ambayo imekuwa ikiongezeka mara kwa mara.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Bw. Ally Iddi amesema awali walikuwa wanauziwa mtungi wa gesi wenye ujazo wa kilo 32 kwa sh. 70,000 na sasa umeongezeka hadi sh. 98,000 kiasi ambacho ni kikubwa ukilinganisha na uzalishaji wao. “Nimeulizia kwenye baadhi ya maduka na kukuta mtungi wenye ujazo kama huo unauzwa sh. 75,000,” alisema.
Kijana mwingine ambaye ni mkaangaji wa samaki, Bw. Mwanya Selemeni alisema hivi sasa hali ya soko la feri ni nzuri tofauti na walivyokuwa wakitumia kuni kwa sababu hakuna moshi. Alimuomba Waziri Mkuu ahakikishe wanafikishiwa gesi ya kutoka Mtwara ili gharama ziweze kupungua.
Mfanyabiashara mwingine wa soko hilo, Bi. Mariam Samweli ambaye alikuwa akiuza kuni na sasa yeye na wenzake wanataka kufanya biashara nyingine lakini banda walilokuwa wakilitumia halina umeme licha ya kuwa wameomba mara nyingi. “Tunaomba kupatiwa umeme ili tuweke vipepeo tuweze kufanya biashara nyingine,” alisema.
Waziri Mkuu pia alitembelea eneo la mnada wa kuuza samaki sokoni hapo ambako alielezwa matatizo ya umeme na uzibaji wa mitaro ya maji machafu hali ambayo inatishia usalama wa afya zao.
“Kuna jipu la umeme hapa, tunachangishwa hela na kumpa mtu ambaye hatumjui lakini hatujawahi kuona risiti, wao wanaweka umeme juu kwa juu na umeme wenyewe wala haukai. Mita tunayo hapa lakini hata namba hatujapewa,” alisema Bw. Omari Masoud kwa niaba ya wenzake.
Kuhusu tatizo la uzibaji mitaro na kutiririsha majitaka, kiongozi wa mama lishe sokoni hapo, Bi. Fatma Ally aliomba watatuliwe tatizo hilo ambalo limedumu kwa zaidi miezi miwili.
Akijibu kero zao, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Raymond Mushi asimamie suala la kuweka umeme kwenye hilo banda pamoja ahakikishe mama lishe wa soko hilo upande wa mnadani waanze kutumia majiko ya gesi badala ya mkaa.
Kuhusu mitaro, alimwagiza meneja wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi aimarishe uzibuaji wa mitaro katika soko hilo. “ Mwambie mkandarasi azibue mitaro kila siku jioni na watumiaji wa soko waache kutumia mifuko ya plastiki kwa sababu inapoingia kule inaziba na wala haiozi,” alisema.
Aliwataka wafanyabiashara waimarishe usafi kwa sababu ni sehemu ya chakula. “Lengo letu ni kufanya soko hili liwe kwenye viwango vya kimataiafa ili mteja anapokuja kununua samaki wabichi ama wa kukaanga awe na chaguo,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa soko hilo, Bw. Mushi alisema bodi ya soko hilo ambayo imeundwa hivi karibuni itakutana kesho kwa mara ya kwanza na miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU