Na Rajab Mkasaba Ikulu, Zanzibar
MTAZAMO wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kufanya mageuzi makubwa ya kilimo kwa kutumia nyenzo bora, mbolea na utaalamu na kufikia uzalishaji wa chakula hadi kuweza kuuza ziada ya chakula hicho kwa lengo la kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa msimu wa mpunga kwa mwaka 2011-2012 Zanzibar uliofanyika huko Cheju, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika hotuba yake, mara baada ya kufanya uzinduzi huo uliohudhuriwa na wakulima wa bonde hilo na mabonde mengine ya mpunga pamoja na wananchi na viongozi mbali mbali wa vyama na serikali wakiwemo wakuu wa Mikoa yote ya Unguja, Dk. Shein alieleza kuwa lengo ni kukifanya kilimo kiwe na tija zaidi.
Dk. Shein, alisema kuwa kupitia Shirika la Chakula (FAO) duniani na mashirika mengine likiwemo la IFAD, nchi zote duniani zimeshajiishwa kulima chakula chake wenyewe. Alisema kuwa dunia imebadilika na tayari kumejitokeza matatizo ya kiuchumi ambapo imepelekea hali kutokuwa tulivu kutokana na kupanda kwa bei ya chakula, matumizi ya fedha yamebadilika na kufanya matumizi hayo kutotabirika.
Dk. Shein alisema kuwa kilimo ndio njia pekee iliyo sahihi ya kumpatia mwanaadamu mahitaji yake ya chakula cha aina yoyote na ni jambo ambalo linafanyika ulimwengu mzima ambapo kwa hivi sasa kilimo kimebadilika ikifananishwa na hapo zamani.
Alieleza kuwa matarajio ya serikali ni kuibadilisha Cheju katika sekta ya kilimo cha mpunga na kulifanya bonde la kilimo cha kisasa cha mpunga kwa heka zake zote 3000, ambapo Cheju itakuwa tofauti na zamani kwani itaweza kuchangia uzalishaji wa zao la mpunga na kuweza kutoa chakula kwa Zanzibar. Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein aliwataka wakulima wa bonde hilo pamoja na mabonde mengine ya mpunga nchini kufuata maagizo yanayotolewa na Wizara pamoja na serikali.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa kuna haja kwa wakulima wa bonde hilo kupanda mbegu moja ili iwe rahisi wakati wa mavuno na kueleza kuwa azma ya serikali ni kuhakikisha mbegu bora, mbolea na utaalamu unatumika katika kilimo kwenye bonde hilo.
Alisema kuwa matarajio ya kupata tani 5000 za mpunga kutoka katika bonde hilo yanawezekana kutokana na juhudi za makusudi zinazochukuliwa kwani mipango yote tayari imeshapangwa ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora za kilomo.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kuna malengo ya kukiimarisha kilimo cha mpunga na kuwa kilimo cha biashara kutokana na matumizi bora ya nyenzo za kilimo kwani serikali imeamua kufanya mabadiliko ya kilimo kwa kukifanya kilimo kiwe cha uhakika zaidi.
Dk. Shein alitoa pongezi kwa mafundi wa matrekta wa Unguja na Pemba na kuitaka Wizara ya Kilimo na Maliasili iwazawadie kutokana na juhudi walizochukua za kuyatengeneza matreka 21 ambapo kwa Unguja 14 na Pemba 7, ambayo yote yako madhubuti na yanafanya kazi.
Pia, alitoa pongezi kwa vikundi vya wakulima wa Cheju kwa kuchangia asilimia 80 na kupelekea kuanza kulimiwa bonde lao. Ameeleza kuwa miongoni mwa ahadi alizoahidi wakati akipita katika bonde hilo kwenye ziara zake za Mikoa tayari zimeshafanyika ikiwa ni pamoja na kupeleka umeme katika bonde hilo.
Alieleza kuwa changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama katika bonde hilo inaendelea kufanyiwa kazi na hivi karibuni itatatuliwa. Aidha, alitoa pongezi kwa Wizara, Masheha na Wakulima kwa kukubali kufanya mabadiliko ya kilimo cha mpunga.
Dk. Shein alimpa nafasi Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Masoud kueleza juu ya mikakati iliyopo ya ujenzi wa barabara ya Jendele-Cheju-Unguja Ukuu Kaebona yenye kilomita 11, ambapo waziri huyo alieleza kuwa mchakato wa ujenzi huo unafanyiwa kazi na hivi karibuni atapatikana mkandarasi wa kuijenga barabara hiyo itakayokuwa na kiwango cha lami.
Alisema kuwa barabara hiyo ni miongoni mwa barabara tatu ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami chini ya Mkopo nafuu wa Benki ya Maendeleo Afrika BADEA kwa mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiwemo barabara ya Koani-Jumbi na Kizimbani- Kiboje.
Nae Kaimu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban aliwataka wakulima kuiunga mkono Wizara ya Kilimo na Maliasili.
Naibu Katibu Wizara ya Kilimo Juma Ali Juma, akitoa ufafanuzi juu ya maandalizi ya kilimo kwa msimu huu alisema kuwa Wizara imeshafanya maandalizi ya kuagiza mbegu ya kutosha kwa msimu huu wa kilimo.
Alisema Wizara yake imeshaagiza mbegu Tanzania Bara kwa ajili ya kugaiwa wakulima ambapo pia, imeshanunua mbegu tani 141. Aidha amesema ahadi zote zilizoahidiwa na serikali zitatekelezwa sanjari na kufanya maandalizi ya mbegu ya NERICA.
Alieleza kuwa katika msimu huu, Wizara imeamua Jumuiya za wakulima wenyewe kuwa ndio wasimamizi wa shughuli zote ambapo kwa Unguja na Pemba kuna vituo 20 vimetengwa na kueleza kuwa bonde hilo la Cheju limeteuliwa kuwa eneo tengefu la mbegu. Naibu katibu huyo alieleza kuwa mwaka ujao eneo lote la bonde hilo litakuwa la kilimo cha umwagiliaji maji ambapo tayari wataalamu kutoka Korea wameshawasili.
Nao wakulima wa mpunga wa Zanzibar katika risala yao walieleza kufarajika kwao na jinsi Dk. Shein anavyosimamia na kukipa kipaumbele kilimo cha mpunga ambapo kwa muda mfupi katika uongozi wake ameweza kushiriki katika shughuli mbali mbali za kilimo hicho. Wakulima hao walitoa pongezi kutokana na Bajeti ya Wizara ya Kilimo ilivyowaona wakulima kwa kuwapatia ruzuku ya pembejeo isiopungua asilimia 75.
Aidha, walieleza changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na tatizo la ujenzi kwenye mabonde ya mpunga na kuiomba serikali kutunga sheria itakayozuia ujenzi katika mabonde ya mpunga sanjari na kueleza kilio chao cha kutaka kutengenezewa barabara zao za ndani mashambani pamoja na kupatiwa maji safi na salama mabondeni mwao.
Dk. Shein katika uzinduzi huo mapema aliyakagua matreka 14 yaliyofanyiwa matengenezo makubwa na mafundi wa karakana ya Mbweni mjini Unguja na kuzindua rasmi shughuli hiyo.