SMZ Yahimiza Kilimo cha Kisasa Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Viongozi na Watendaji katika Ofisi za Serikali Mkoa wa Mjini Magharibi alipomaliza ziara yake kwa mkutano wa majumuisho katika ukumbi wa Chuo cha Karume Mbweni Nje ya Mji wa Unguja. {Picha na Ramadhan Othman, Ikulu}

Baadhi ya Viongozi katika Ofisi za Serikali Mkoa wa Mjini Magharibi wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipozungumza nao katika mkutano wa majumuisho ya ziara yake aliyoifanya katika Mkoa huo, ukumbi wa Chuo cha Karume Mbweni. {Picha na Ramadhan Othman, Ikulu}


Na Said Ameir, Ikulu Zanzibar

LENGO la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuwaondoa wakulima kutoka kilimo cha kutegemea mvua hadi kilimo cha kisasa cha umwagiliaji maji.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewaambia wakulima wa bonde la Kizimbani Wilaya ya Magharibi jana kuwa ufumbuzi wa tatizo la uharibifu wa mazao kutokana na ukosefu wa mvua ni kubadili kilimo kuwa cha umwagiliaji.

Dk Shein alifika katika bonde hilo, katika siku yake ya pili ya ziara ya kutembea mikoa mitano ya Zanzibar, kukagua uharibifu wa kilimo cha mpunga ulioathirika kutokana na ukosefu wa mvua ambao ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi.

“kilimo hiki cha kutegemea mvua hakina muamana…si cha kutegemea…mvua haikunyesha kwa wakati mazao yamevia na hiya ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi”alisema Dk Shein.

Kwa hivyo aliwaambia wananchi hao kuwa Serikali inajua kuwa suluhisho la tatizo hilo ni kilimo cha umwagiliaji ambapo alisema “bila ya maji hakuna kilimo…bila ya mbegu bora hakuna kilimo…tunahitaji madawa ya kuulia wadudu, mbolea matrekta, vifaa vya kisasa vya kuvunia mazao” Dk Shein alieleza na kusisitiza kuwa hayo ndio mahitaji ya kilimo cha kisasa.

Aliwaeleza wananchi hao kuwa baadhi ya vifaa hivyo vipo tayati nchini ingawa havitoshelezi na kubainisha kuwa vifaa hivyo vimeanza kutumika na tayari wananchi wa baadhi ya maeneo ya mashamba wameshaanza kufaidika navyo kutoka na matokeo mazuri ya kilimo cha mazao yao.

Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali yake imeamua na tumejidhatiti kukibadili kilimo ndio maana Serikali inagharimia asilimia 75 ya gharama za mbegu, madawa na mbolea ili kuwapunguzia wakulima mzigo wa gharama za kununulia vitu hivyo na kueleza kuwa Serikali imeweka lengo kwa awamu ya kwanza kulibadili eneo la hekta 8,000 kuwa la kilimo cha umwagiliaji.

Dk. Shein aliwaambia wananchi hao hatua hiyo imelenga kuiwezesha Zanzibar ifikapo mwaka 2015 kipindi cha ndani ya miaka miwili ijayo kujitosheleze kwa asilimia 50.

Alibainisha kuwa tatizo kubwa katika eneo bonde la Kizimbani ni maji ambapo Serikali inaweza kulazimika kuchimba visima ili kutekeleza ombi la wakulima wa bonde hilo la kutaka eneo lao liwemo katika mpango wa kilimo cha umwagiliaji.

Wakati huo huo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Bwana Affan Said alieleza wananchi wamekuwa wakitumia uzoefu wao wa asili kutambua vipindi vya mvua na kwamba viashiria/alama wanazozitumia haziendani tena na wakati sasa ambapo kuna mabadiliko ya tabia nchi.

Tatizo la kuharibika kwa mazao hasa mpunga aliongeza Katibu Mkuu huyo liko zaidi kisiwani Unguja kuliko kisiwa cha Pemba lakini jitihada zinafanyika kuwasaidia wakulima waliopatwa na kadhi hiyo mbegu za muda mfupi ili waweze kuendeleza kilimo hivi sasa.

Awali Rais wa Zanzibar na Mweneyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitembelea kituo cha kutolea mafunzo ya kilimo maalum cha mbogamboga kinachoendeshwa na Kampuni ya Ujenzi ya RANS huko Kombeni.