Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta amemwita katika bunge hilo Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi aje kueleza alichokisema katika kanisa moja juzi, kauli ambayo inadaiwa kuwaudhi wabunge toka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao ni wajumbe wa Bunge la Katiba waliogoma kuhudhuria vikao vya bunge hilo tangu jana.
Lukuvi ambaye leo amefika bungeni mjini Dodoma, akizungumza katika bunge hilo alikiri kusema maneno ambayo aliyaita ni hofu yake yeye binafsi endapo mfumo wa Serikali tatu utapitishwa juu ya uwezekano wa Jeshi kuchukua nchi kwa kile alichokiita endapo litashindwa kuhudumiwa na Serikali ya Muungano.
Alisema alichokizungumza juzi ni hoja yake juu ya uwepo wa mfumo wa Serikali tatu, huku Serikali ya Muungano ikionesha wazi haina vyanzo vya mapato ya uhakika zaidi ya kutegemea kuwezeshwa kutoka kwa Serikali za Tanganyika na Zanzibar jambo ambalo alisema ni hatari kwa mtazamo wake.
Alisema Serikali ya Muungano licha ya kutokuwa na uwezo kifedha imepewa vyombo vya ulinzi yaani majeshi kuyasimamia, chombo ambacho ni nyeti na huitaji bajeti kubwa kutokana na shughuli zake. Alisema endapo Serikali ya Muungano itashindwa kulihudumia jeshi ni rahisi kuchukua nchi hiyo kujikuta taifa linaingia katika hali ya utawala mwingine.
Alisema haoni sababu ya kujaribiwa kwa mfumo wa Serikali tatu kuingizwa katika katiba kwa kuwa unaonesha hofu kwake na wengine wengi, hivyo ni bora mfumo wa Serikali mbili ukaboreshwa na kuendelea kutumika kwani hauna hofu yoyote na umeonekana unafaa.
Aidha aliongeza kuwa uwepo mfumo wa Serikali tatu huenda ukaibua hali ya ubaguzi kutokana na kuwa na Watanganyika na Wazanzibari tofauti na ilivyo sasa, jambo ambalo linaweza kuchochea itikadi za kibaguzi ama wa utaifa, kidini na hata kimakabila. Alisema alichokisema ni hofu anayoiona yeye katika mfumo huo wa Serikali tatu hivyo atasema popote bila woga kwani anakiamini anachokisema.
“…Sasa kama waliogoma wamegoma kwasababu ya mimi kusema hofu yangu na waendelee kugoma…lakini mimi nitasema muda wote bila woga kwa kuwa hii ni hofu yangu kama wao hawana hofu hiyo ni shauri yao…,” alisema Lukuvi.
Hata hivyo akifafanua zaidi alisema malalamiko yanayotolewa kuwa kauli aliyoitoa ni ya kichochezi hayana msingi kwani kama ni kutoa kauli za kichochezi basi zinatolewa na Chama cha CUF chenyewe kwani hivi karibuni kiongozi wao mkuu Zanzibar alitoa kauli ya uwongo na kichochezi ya kumlisha maneno Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa aliwatisha wananchi jambo ambalo si la kweli.
“…Katika hali hii anayestahili kuitwa mchochezi ni nani, wao au mimi,” alihoji Lukuvi na kuendelea kufafanua kuwa maneno aliyoyasema yeye yamekuwa yakirudiwa mara kadhaa na viongozi wengi akiwemo Mwenyekiti wa TLP alipokuwa akizungumza lakini hawakugoma nyuma hadi yeye alipozungumza maneno kama hayo juzi.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti Sitta amesikitishwa na kitendo cha UKAWA kutoka nje ya bunge kwa mgomo kwani madai yao yangeliweza kuwasilishwa katika utaratibu uliopo na kusikilizwa kisha maridhiano kupatikana. Aliwataka viongozi wa kundi hilo kurudi bungeni na waendelee na kazi ya kutunga katiba kwani kama kuna jambo lolote ambalo wanaona linawakwaza waliwasilishe ofisi ya mwenyekiti na litashughulikiwa.
Hata hivyo, kauli iliyonukuliwa leo toka kwa Freeman Mbowe ambaye ni mmoja wa viongozi waliogomea bunge la Katiba amesema hawapo tayari kurudi bungeni kwa sasa kwani hawawezi kukubali CCM wafanye wanavyotaka katika mchakato huo huku wao wakionekana hawasikilizwi hoja zao.
Sitta tayari ameitisha kikao cha kamati ya uongozi kujadili suala hilo na kuomba wajumbe ambao wapo katika kamati hiyo na wamegoma wajitokeze kwenye kamati yao na waeleze hoja yao ili kutafuta maridhiano.