Sitta aitaka benki ya NMB kufungua matawi nchi za A. Mashariki

Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

Na Mwandishi Wetu, Arusha

WAZIRI wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ameitaka Benki ya NMB kufungua matawi yake kwenye nchi za Afrika Mashariki ili kupanua biashara zake nje ya mipaka ya Tanzania.

Sitta alisema kuwa benki ya NMB, ambayo ni benki kubwa kuliko zote hapa Tanzania, sasa ina uwezo mkubwa wa kufanya biashara hata nje ya Tanzania.

“Nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ziko kwenye mchakato wa kuwa na sera ya pamoja ya masuala ya masoko ya hisa, uwekezaji na kuruhusu mitaji iweze kuhamishwa kutoka nchi moja mpaka nyingine,” alisema Sitta.

Waziri huyo alitoa rai hiyo jijini Arusha jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa kifedha na masuala ya kibenki ulioandaliwa na benki ya Rabbobank ya Uholanzi na NMB. Benki ya Rabobank ina hisa asilimia 35 kwenye benki ya NMB.

Sitta alisema kuwa nchi wanachama wa EAC – Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi – zinajafanya kazi kwa pamoja kuongeza ushirikiano kati ya masoko ya hisa na fedha ya nchi hizo.

“Kutokana na mazingira haya ya kuvutia, ninatoa wito kwa NMB kupanua huduma zake nje ya Tanzania. Tunataka kuiona NMB katika siku chache zijazo ikitoa huduma zake pia kwenye nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na kusini Sudan,” alisema.

Alisema tangu kubinafsishwa kwa NMB, benki hiyo imetoa mchango mkubwa kuendeleza sekta za kilomo na wafanyabiashara wadogo nchini kote kutokana na kuwa na mtandao mkubwa wa zaidi ya matawi 140.

Wataalamu wapatao 100 wa masuala ya kibenki wanahudhuria mkutano huo wa mwaka ulioandalia Arusha Okt. 26-28 na Rabbobank ikishirikiana na NMB.
“Tumefurahi sana kuona kuwa Rabbobank, moja ya benki zinazoongoza duniani, imeamua kufanya mkutano huu muhimu hapa Tanzania,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Mark Wiessing.

“Tupo tayari kutoa mchango muhimu kwenye kuhakikisha kuwa wakulima wadogo na ushirika wanapata huduma za kifedha.”

Naye mwakilishi wa Rabobank kutoka Uholanzi, Diane Boogaard, alisema: “Tume kuja na wataalamu kutoka America, ulaya na Asia ili waje kuona wenyewe fursa ambazo zipo hapa.”