Sitanyamazia Kushambuliwa Kwangu – Absalom Kibanda

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda (wa tatu kulia) akiwasili jana. Picha na FullShangwe Blog)

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda amerejea chini jana kutoka Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa na kusisitiza kwamba hatanyamaza kuzungumzia janga la kushambuliwa kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Kibanda alisema asingependa kuona jambo hilo linamtokea mwandishi mwingine wa habari.

Kibanda, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, alikuwa akitibiwa huko baada ya kushambuliwa na kuumizwa vibaya na watu wasiofahamika usiku wa Machi 5, mwaka huu.

Alisema kutokana na hali hiyo, waandishi wanapaswa kuwa na mshikamano ili kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayajirudii.

“Waandishi wana nafasi kubwa ya kuliondoa taifa katika hali hii. Waendelee kuandika na kuelimisha wananchi ili nao wasaidie kuzuia ukatili wa aina hii. Hatuwezi kuishi katika nchi ambayo watu wanafanyiwa ukatili mkubwa kiasi hiki halafu wanaachwa hivihivi,” alisema Kibanda.

Kibanda alisema jambo lililomtokea lilikuwa baya kwani alikuwa akipoteza fahamu kila wakati kutokana na maumivu makali.

“Lakini sasa namshukuru Mungu, nimepona, sina maumuvu tena kama yale,” alisema Kibanda na kuelezea kufurahishwa kwake na ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwa wadau wa habari na wananchi kwa jumla.

Ameiomba Serikali kuharakisha ripoti ya uchunguzi wa tukio lake kwa sababu ni muda mrefu umepita na kwamba mpaka sasa hakuna taarifa zozote zilizotolewa.

“Nilipolazwa Muhimbili Kitengo cha Moi, alikuja kuniangalia Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema waliniahidi kushughulikia suala langu ili waliohusika na tukio hili wafikishwe mahakamani,” alisema.

Alisema si hao tu, bali pia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye alikwenda Afrika Kusini kumjulia hali, alimwahidi kuwashughulikia watu waliohusika.

“Sisi sote ni mashahidi wa ukimya ambao upo kwani mpaka sasa watu hao hawajakamatwa, wala hakuna taarifa zozote zinazohusu kufikishwa mahakamani,” alisema.

Kibanda alisema katika miaka ya karibuni, kumekuwa na matukio mbalimbali yanayohusisha kupigwa, kuuawa au kutishiwa maisha kwa waandishi, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa matukio hayo hayaji bure, kuna chanzo chake.

CHANZO: Gazeti Mwananchi