Sita wafariki katika ajali ya basi la wachezaji-Togo.

Kikosi cha timu ya Taifa ya Togo

Watu sita walifariki baada ya basi lililokua likisafirisha wachezaji wa klabu ya mpira wa miguu Etoile Filante kudondoka katika korongo na kushika moto.
Ajali hiyo ilitokea umbali wa maili 100 kaskazini mwa mji mkuu Lome wakati wachezaji hao wanakwenda kupambana na Timu nyingine katika michuano ya Ligi ya Togo.
Pamoja na maofisa sita waliofariki, wengine 25 wamelazwa katika hospitali kwa majeraha makali ya moto.
Miongoni mwa wale waliopoteza maisha yao ni goalkipa wa Timu ya Taifa ya Togo Charles Balogoun.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Togo tairi moja ya basi hilo ilipasuka na kusababisha gari kupoteza njia na kuishia chini kwenye korongo karibu na mji wa Atakpame.
Mchezaji mwingine ambaye ni golikipa aliyenusurika ameliambia shirika la habari Associated Press kuwa “siwezi kuelezea ni jinsi gani tumeponyoka ajali hiyo”alisema Mama Souleyman.
“Wengi wa wachezaji waliponyoka ajali hiyo kwa sababu walikaa safu ya mbele ya basi hilo.”
Picha zilizopeperushwa kwenye runinga ya Togo zilionyesha mabaki ya basi lililochomeka kabisa.
Rais wa Togo Faure Gnassingbe ameamuru waliojeruhiwa katika ajali hiyo wahamishiwe katika hospitali ya kijeshi mjini Lome.
Ni mwaka jana tu ambapo wachezaji wawili wa Timu ya Taifa ya Togo waliuawa wakati Timu yao ikisafiri wakati wa mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola. Basi lao lilifyatuliwa risasi na kundi la waasi wanaoipinga serikali ya Angola.
Mnamo mwaka 2007, Waziri wa michezo wa Togo Richard Attipoe alikua miongoni mwa watu 22 walipoteza maisha yao helikopta iliyowasafirisha yeye pamoja na mashabiki wa Timu ya Taifa kupatwa na ajali nchini Sierra Leone. Hii ilikua ni wakati wa michuano ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika.

-BBC