SIRI nzito imeibuka sakata la madai ya madereva wa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo imeelezwa kuwa wabunge wanaoogoza kuwatimu madereva wao ni wa vyama vya upinzani ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao baadhi yao wamekuwa wakijiendesha wenyewe na kushindwa kupeperusha bendera ya bunge.
Inadaiwa mbunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) na mbunge Zitto Kabwe ambaye ni Waziri kivuli wa fedha na uchumi (Chadema) wakiibuka kuwatetea madereva hao kuwa wanapaswa kulipwa vizuri kama ambavyo wabunge wenzao wamekuwa wakijitetea kuhusu maslahi mazuri Kwao wafanye hivyo hata kwa kupigania bungeni maslahi mazuri ya madereva wao badala ya kuwapunja haki zao.
Filikunjombe ambaye amekuwa mbunge wa kwanza katika bunge hilo kufunguka kuguswa na malalamiko hayo ya madereva na hata kuwaunga mkono madereva hao kwa kuwataka kuondoa uoga katika kupigania maslahi yao.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungunza na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na Madai hayo ya madereva na kudai kuwa amesikitishwa sana kuona madereva wakiendelea kupunjwa haki zao wakati kazi wanazozifanya za kuwaendesha wabunge hao ni kubwa zaidi na kuwataka wabunge wenzake kuwa na roho za huruma kwa madereva hao.
Hata hivyo alishauri wabunge wenzake kujaribu kuwatetea madereva wa wabunge ili Kama inawezekana basi madereva hao waweze kulipwa kama madereva wa mawaziri badala ya posho na Mishahara yao kupitia kwenye akaunti za wabunge.
” Mimi ninawsunga mkono madereva na nitaendelea kufanya hivyo hadi watakavyotendewa haki …hoja ya madereva kuhusu ajali za Mara kwa Mara kwa wabunge wanaojiendesha wenyewe ni ya Msingi zaidi na wabunge wenzangu wanapaswa kuifanyia kazi kuacha kufanya kazi ya udereva hata Kama ni dereva”
Kwa upande wake Mbunge Zitto Kabwe alisema kuwa madereva wanapaswa kuendeleza moto huo ambao wameuwasha bila kuchoka na kuwa tabia ya madereva hao wamekuwa wakianzisha suala hilo na kabla ya kufika mwisho wamekuwa wakiliacha hewani.
Zitto alisema kwa safari hii ataungana nao kupigania maslahi yao na kuwataka madereva hao kuendelea kujenga hoja zaidi ili kuweza kutendewa haki bila ya kugombana na wabunge hao ambao ni mabosi wao.
Alisema kuwa kuanzia mwezi ujao kila mbunge atapewa kiasi cha shilingi 170,000 kwa ajili ya kumlipa dereva wake kila mwezi na kuwa ni vema fedha hizo wabunge kuingia mikataba na madereva hao na mikataba hiyo Kusainiwa na katibu wa bunge ili iwe ya kisheria na fedha hizo kuingizwa moja kwa moja katika akaunti zao.
Zitto alithibitisha Madai ya madereva hao kuwa ni kweli Kabisa wabunge wengi katika bunge hilo hawana madereva na wamekuwa wakila fedha ndogo ambavyo zimekuwa zikitolewa na bunge kwa ajili ya madereva.
Alisema kuwa kwa kuwa mbunge amekuwa akilipwa kiasi cha shilingi 80,000 kwa siku kwa ajili ya posho ni vema kuwepo utaratibu wa kumlipa dereva wake nusu ya fedha hizo kwa kazi anayoifanya badala ya wabunge kuwalipa shilingi 20000 ama chini ya hapo
Zitto alisema kuwa kazi ya madereva ni kubwa hivyo wabunge wanapaswa kuacha mchezo katika kutambua kazi ya madereva hao na kuachana na ubaili usio na maana katika kuwalipa haki stahiki .
“…nasema nitasimama kidete kutetea haki za madereva ili kuona nao wanatendewa haki…suala hilo la madereva kulalamika juu ya maslahi duni kwa mara ya kwanza lilipoibuka zaidi ya miaka miwili sasa mimi niliungana nao kuwatetea na sasa nitaendelea kufanya hivyo,”
Kuhusu Madai ya wabunge wengi wa Chadema kuongoza kutimua madereva na kujiendesha wenyewe na baadhi ya wabunge wa viti maalum kuendeshwa na waume zao, Zitto alitaka wabunge hao pia kuhojiwa wenyewe badala ya kuwasemea yeye. Mbali ya wabunge wa majimbo kujiendesha kwa upande wa wabunge wa viti maalum wamekuwa wakiendeshwa na waume zao huku baadhi yao wakilala kitanda kimoja zaidi ya watatu imefahamika.
Mmoja Kati ya wabunge wa viti maalum wa vyama vya upinzani amedokeza Siri nzito hiyo kwa wabunge na kudai kuwa wabunge hao wamekuwa wakifanya hivyo kwa kuishi maisha ya gheto wawapo bungeni Kama njia ya kubana matumizi .
Pia alisema kuwa mbali ya wabunge kushindwa kuwalipa vizuri madereva wao pia sehemu kubwa ya wabunge wameamua kuegesha mashangigi ya ubunge ambayo walikopeshwa na kutumia magari ya hari ya chini zaidi kutokana na mashangingi hayo kuonekana kutumia mafuta mengi zaidi.
Kwani wamedai kuwa njia hiyo itawasaidia zaidi kujua umma kujua jinsi ambavyo wabunge hao wanavyoongoza kuwatetea wanyonge wakati wao wakiendelea kuwatendea ndivyo sivyo madereva wao.
Madereva hao wamesema kuwa wabunge wamekuwa mbele kutetea madereva wanaofanya kazi hiyo hapa nchini kupewa mikataba wakati kwa upande wao wabunge hao wamekuwa wakiendelea kuwafanyia ufisadi kwa kutowalipa fedha zao wala kuingia mikataba ya kisheria.
Uamuzi huo wa madereva hao kutaka kuwaanika katika vyombo vya habari wabunge hao umetolewa leo tena ikiwa ni siku mbili baada ya blog ya Francis Godwin kuandika juu ya madai ya madereva hao kwa mabosi wao ambao ni wabunge.
Mwenyekiti wa chama cha madereva wa wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania Juvenille Joseph alisema kuwa wapo baadhi ya wabunge wachache wa CCM na wale wa vyama vya upinani ambao wamekuwa wakiongoza kwa kuwajali madereva wao .
Ila alisema wapo baadhi ya wabunge ambao madereva wao hata kulala kwao na kula kwao wakiwa bungeni Dodoma ni shida na kuwa baadhi ya madereva wanaolipwa vizuri wamekuwa wakiwachangia fedha za kununua mihogo na maji .
Hivyo alisema kuwa uwazi wa madereva hao kwa kuanika majina ya wabunge wao ambao wamekuwa wakiwapunja haki zao itasaidia kupata haki yao badala ya kuendelea kuwa madereva wa majina na heshima wakati mfukoni hawana kitu.
“Mbali ya wabunge kufanya kazi nao bila mikataba ila baadhi ya wabunge wamekuwa wakilipa vizuri akiwemo bosi wangu Felista Bulla (CCM) mimi kiukweli analipa vizuri sana tofauti na wenzangu ila bado nitaendelea kupigania haki ya madereva wenzangu…,mimi wakati bunge la mwaka 2005 alinipa milioni 3,”
Wabunge wengine waliotoa mkono wa ahsante kwa madereva wao ni pamoja na mbunge, Stella Manyanya (CCM) milioni 5.5, Zitto Kabwe (Chadema) milioni 5.5 na mbunge mmoja wa viti maalum kutoka Zanzibar yeye alimpa dereva wake milioni 3 japo hakurudi bungeni.
“Wabunge wetu wanaongoza kwa kuikosesha serikali mapato yake na ajira kwa vijana kupungua kutokana na baadhi yao kushindwa kutoa mikataba ya kazi wala kuwalipa mishahara ambayo serikali kupitia bunge ilipendekeza kwa ajili ya madereva wa wabunge toka mwaka 2008.”
Hata hivyo alimpongeza mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe (CCM) kuwa ameonekana kuwa mbunge aliyeingia bungeni kwa kipindi hiki cha kwanza na kuwa mfano wa kumjali dereva wake.
Madereva hao walisema kuwa sehemu kubwa ya wabunge hao wameanza kuendesha magari yao wao wenyewe baada ya kushindana na madereva waliokuwa wakiwaendesha awali baada ya kushindwa kuwalipa mishahara na posho zilizobainishwa kisheria na ofisi ya bunge.
Hata hivyo walisema kuwa suala hilo la wabunge kushindwa kuwalipa vizuri madereva si kwa wabunge wa CCM pekee bali ni wabunge karibu wote wakiwemo wa vyama vya upinzani ambao baadhi yao kwa sasa wanajiendesha wenyewe baada ya kukimbiwa na madereva wao kwa kushindwa kuwalipa.
Pia walisema matukio ya ajali kwa wabunge yamezidi kuongezeka kutokana na wabunge hao kushindwa kufanya kazi na madeva na kuishia kuifanya kazi hiyo wao wenyewe na matokeo yake kutokana na mawazo ama kuwa na mambo mengi kichwani wamekuwa wakishindwa kuyamundu magari yao na kuishia kusababisha ajali za barabarani ambazo baadhi ya ajali hizo zimekuwa zikisababisha vifo ama ulemavu kwa wabunge hao.
“Leo ukitazama hapa bungeni Dodoma utaona idadi kubwa ya wabunge wanajiendesha wenyewe kama si mbunge kuwaendesha wenzake basi mbunge amekuwa akijiendesha mwenyewe na wapo wanaokuja na madereva hadi hapa Dodoma na baada ya hapo dereva amekuwa akipewa nauli ya kurudi jimboni na mbunge anaendelea kujiendesha mwenyewe kama njia ya kubana matumizi,”
Aidha walisema kuwa miongoni mwa madereva waliokosa ajira ni pamoja na wale waliokuwa madereva wa mawaziri na manaibu mawaziri ambao hawakurejea tena baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza mabadiliko ya baraza la mawaziri hivi karibuni ambapo mawaziri hao kwa sasa wamegeuka kuwa madereva wenyewe.
Makamu mwenyekiti wa chama cha madereva wa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Adam Said alisema kuwa sababu ya wabunge wengi kukimbiwa na madereva ni kutokana na maslahi duni wanayoendelea kulipwa na kuwa hivi sasa baadhi ya wabunge baada ya kukimbiwa na madereva wamelazimika kuwatumia ndugu zao kama njia ya kukwepa kuwalipa mishahara .
Pia alisema maisha ambayo madereva hao wamekuwa wakiishi mjini Dodoma ni heri ya omba omba kutokana na wabunge hao kuwalipa kiasi cha shilingi 50,000 ama chini ya hapo na kutaka kuitumia kwa muda wa wiki moja ama mwezi mzima jambo lililopelekea madereva hao kupanga vyumba mtaani na kuishi katika chumba kimoja zaidi ya watatu kama sehemu ya kubana matumizi.
Mwenyekiti wa chama cha madereva wa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juvenille Joseph alithibitisha madaia ya madereva hao na kuwa tayari uongozi wake umefikisha malalamiko ya madereva hao katika ofisi ya chama cha wafanyakazi mkoa wa Dodoma pamoja na ofisi ya spika wa bunge Anne Makinda ili kushughulikia madai hayo.
Alisema kuwa kwa sasa wanakusudia kuitisha mkutano wa dharura wa madereva wote wanaowaendesha wabunge ili kuweza kuwa na msimamo wa pamoja katika kupigania haki zao na baada ya hao watawatumia barua wabunge ambao wanajiendesha wenyewe ili waweze kujiunga na chama hicho cha madereva wa wabunge .
Kwani alisema kuwa katika barua iliyotolewa na ofisi ya bunge Novemba 3 mwaka 2008 barua yenye kumbukumbu namba FA.155/206/01/70 ikiwa na kichwa yahusu posho ya ubunge Malimbikizo July–Octoba 2008 ilibainisha posho na mishahara hiyo.
Joseph alisema kuwa posho ya mafuta lita 1000 kwa lita shs 2500 kwa wakati huo ilikuwa ni kiasi cha shs milioni 2.5 kwa mwezi, Matengenezo yagari asilimia 40 ya thamani ya mafuta ambayo ilikuwa ni milioni 1 kwa mwezi, posho ya dereva siku 10 kwa shilingi 30,000 (vijijini ) ilikuwa ni shilingi 300,000 na posho ya mbunge siku 10 kwa kila atakazokuwepo kijijini kwa kila siku shs 45,000 ilikuwa ni shs 450,000 huku mshahara wa dereva kwa mwezi ulikuwa ni shs 100,000 na kufanya jumla kwa mwezi kuwa bajeti ya shs milioni 5,115,000 kwa wakati huo.
Ila pamoja na sasa posho za wabunge kupanga ila bado wabunge wamekuwa wakiwalipa madereva wao kiasi cha shs 70,000 hadi 90,000 kwa mwezi fedha ambazo haitoshi kwa maisha ya sasa hivyo kutaka fedha za madereva kuingizwa katika akaunti zao na madereva wote wa wabunge kuwa na mikataba ya kazi badala ya kuendelea kufanya kazi kirafiki na kindugu.
Chanzo: Francis Godwin Blog