Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Ligi imeagiza mchezaji Patrick Mafisango wa Simba aandikiwe barua ya onyo kutokana na kumsukuma mwamuzi Isihaka Shirikisho baada ya kumuonesha kadi nyekundu mchezaji mwenzake Haruna Moshi kwenye mechi kati ya Simba na JKT Oljoro.
Nayo klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kurusha makopo ya soda na chupa za maji wakipinga uamuzi wa mwamuzi Shirikisho kumtoa kwa kadi nyekundu Haruna Moshi.
Wachezaji waliopigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kutokana na kupiga ambapo pia wanakosa mechi tatu za ligi kwa mujibu wa Kanuni ya 25 ni nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na Cyprian Lukindo wa Villa Squad.
Wakati huo huo, inaripotiwa kuwa pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Azam lililochezwa Februari 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 67,548,000.
Jumla ya watazamaji 19,257 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 117 kwa kiingilio cha sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000 kwa VIP A.
Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 10,303,932.20 kila timu ilipata sh. 13,182,800.34, uwanja sh. 4,394,266.78.
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,757,706.78, TFF sh. 4,394,266.78, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,197,133.39, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 439,426.78 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 4,394,266.78.
Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. wamuzi wa akiba sh. 30,000, tiketi sh. 4,350,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.
Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 1,347,990,280 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 1,555,420.