Simba Yapata Naasi ya 3 Kombe la Uhai

Simba imetwaa nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu zenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuitandika Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 3-0.
Hadi mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam, Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Mabao yote ya washindi katika mechi hiyo yalifungwa na Ramadhan Mkipalamoto. Mfungaji alifunga bao la kwanza dakika ya 43 wakati mengine alipachika dakika za 57 na 70. Kwa kunyakua nafasi ya tatu, Simba imeondoka na kitita cha sh. 500,000.
Mechi ya fainali ya michuano hiyo kati ya Azam ya Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga itachezwa leo (Desemba 23 mwaka huu) saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Mbali ya kombe, bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai atapata sh. milioni 1.5 wakati makamu bingwa atazawadiwa sh. milioni 1.
Timu iliyoonesha zaidi mchezo wa kiungwana (fair play) itapata sh. 400,000, mchezaji bora wa mashindano sh. 350,000, mfungaji bora sh. 300,000 na kipa bora sh. 300,000. Naye kocha bora katika mashindano hayo atazawadiwa sh. 300,000 kama itakavyokuwa kwa refa bora.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI MUSA RICO
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Coastal Union, Musa Rico kilichotokea jana (Desemba 22 mwaka huu) jijini Tanga.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti akiwa mchezaji Rico, na baadaye kocha alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea na kufundisha ikiwemo Coastal Union, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Rico, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) na klabu ya Coastal Union na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko yanatarajiwa kufanyika leo (Desemba 23 mwaka huu) mkoani Tanga. Mungu aiweke roho ya marehemu Rico mahali pema peponi. Amina
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA TAREFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Desemba 22 mwaka huu).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Tabora.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TAREFA chini ya uenyekiti wa Yusuf Kitumbo aliyeshinda kwa kura 16 dhidi ya nane za Musa Ntimizi, na Paul Werema ambaye hakupata kura.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Tabora kwa kuzingatia katiba ya TAREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Yusuf Kitumbo (Mwenyekiti), Fate Remtulla (Katibu), Dick Mlimuka (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Razak Irumba (Mwakilishi wa Klabu TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Eric Kabepele na Mwalimu Sizya.
TWFA YAWATUZA TENGA, FURAHA FRANCIS
Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake Tanzania (TWFA) kimetoa tuzo kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na Meneja wa timu ya Taifa (Twiga Stars), Furaha Francis kutokana na mchango wao katika kuendeleza mchezo huo.
Tuzo hizo zilitolewa katika Mkutano wa Uchaguzi wa TWFA uliofanyika Desemba 19 mwaka huu mjini Morogoro kutokana na mchango wao katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wanawake nchini.
“Ni dhahiri kazi ya kuendeleza soka ya wanawake ni wajibu wa Shirikisho (TFF), lakini Rais wa TFF alitoa kipaumbele zaidi na alijitoa kuhakikisha misingi imara ya kuendeleza soka ya wanawake inawekwa,” alisema Mwenyekiti wa TWFA, Lina Kessy.
Pia Mkutano huo ulitambua na kumpa tuzo Furaha Francis ambaye amekuwa Meneja wa Twiga Stars kwa miaka minane mfululizo. Licha ya kuwa Meneja wa Twiga Stars, ametumia muda wake na kujitoa katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wanawake.
TWFA itaendelea kutumia michango yao katika mpira wa miguu kwa wanawake nchini.