Simba, Yanga Zavuna Mil 123 Kila Moja Mgao wa Mapato ya Pambano Lao

Simba, Yanga Zavuna Mil 123 Kila Moja Mgao wa Mapato ya Pambano Lao

Simba, Yanga Zavuna Mil 123 Kila Moja Mgao wa Mapato ya Pambano Lao

MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ya watani wa jadi Simba na Yanga iliyochezwa jana (Oktoba 20 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 imeingiza sh. 500,727,000.
 
Washabiki 57,422 ndiyo waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 63 kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000. Ni tiketi 131 tu ndizo hazikuuzwa ambazo ni 90 za VIP A, 40 za VIP B na moja ya VIP C. Tiketi zilizochapwa kwa ajili ya mechi hiyo ni 57,558 ambayo ndiyo idadi ya viti vilivyopo kwenye uwanja huo.
 
Kila klabu imepata mgawo wa sh. 123,025,564.32 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,382,084.75.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 62,555,371.69, tiketi sh. 7,309,104, gharama za mechi sh. 37,533,223.01, Kamati ya Ligi sh. 37,533,223.01, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 18,766,611.51 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 14,596,253.39.

VPL YAPISHA MECHI YA U20 WANAWAKE
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya marekebisho ya ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ili kupisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania na Msumbiji.
 
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza kwa mashindano ya wanawake wenye umri chini ya miaka 20 itachezwa Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.
 
U20 tayari imehamishia kambi yake hosteli ya Msimbazi Center, Dar es Salaam kutoka JKT Ruvu mkoani Pwani tangu wiki iliyopita kujiandaa kwa mechi hiyo. Fainali za Kombe la Dunia kwa U20 wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada.
 
Marekebisho ya ratiba ya VPL yamegusa raundi zote tatu zilizobaki kukamilisha mzunguko wa kwanza. Kutokana na marekebisho hayo mechi za raundi ya 11 zitakuwa ifuatavyo; Oktoba 28 mwaka huu ni Coastal Union vs Mtibwa Sugar, Oljoro JKT vs Ashanti United, Ruvu Shooting vs Kagera Sugar na Simba vs Azam. Oktoba 29 mwaka huu ni Tanzania Prisons vs Mbeya City, Yanga vs Mgambo Shooting na Rhino Rangers vs JKT Ruvu.
 
Raundi ya 12 ni kama ifuatavyo; Oktoba 31 mwaka huu ni Simba vs Kagera Sugar, Novemba 1 mwaka huu ni JKT Ruvu vs Yanga. Novemba 2 mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Coastal Union, Tanzania Prisons vs Oljoro JKT, Azam vs Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar vs Rhino Rangers na Mbeya City vs Ashanti United.
 
Raundi ya 13 ni kama ifuatavyo; Novemba 6 mwaka huu ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashanti United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar. Novemba 7 mwaka huu ni Azam vs Mbeya City.
 
Mechi za kufunga raundi ya 10 zitachezwa keshokutwa (Oktoba 23 mwaka huu) kama ratiba inayoonesha. Mechi hizo ni kati ya Coastal Union vs Simba, Tanzania Prisons vs Kagera Sugar na Yanga vs Rhino Rangers.
 
VITAMBULISHO MICHUANO YA CHALENJI
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limefungua maombi ya vitambulisho (Accreditation) kwa ajili ya waandishi wa habari wanaotarajia kuripoti mashindano ya Kombe la Chalenji.
 
Mashindano ya Kombe la Chalenji yatafanyika nchini Kenya kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu. Kwa waandishi wa habari wanaotaka kuripoti mashindano hayo wanatakiwa kutuma maombi yao kabla ya Oktoba 31 mwaka huu. Mbali ya majina, katika maombi hayo mwandishi wa habari ni lazima aoneshe chombo anachofanyia kazi na kuambatanisha na picha moja ya pasipoti.
 
Boniface Wambura Mgoyo, Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)