Na Mwandishi Wetu
YANGA na Simba ni miongoni mwa timu nne zitakazokuwa viwanjani kesho (Machi 31 mwaka huu) kusaka pointi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ambayo iko katika raundi ya 22.
Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi namba 148 kati ya Coastal Union na Yanga. Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Rashid Msangi wa Dodoma ambaye atasaidiwa na Rashid Lwena (Ruvuma) na Issa Malimali (Ruvuma).
Mwamuzi Amon Paul wa Musoma ndiye atakayechezesha mechi namba 151 kati ya African Lyon na Simba itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio kwenye mechi ya African Lyon na Simba ni sh. 3,000 kwa viti vya kijani na bluu, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati VIP A ni sh. 15,000.
Aprili Mosi mwaka huu kutakuwa na mechi ya VPL kati ya Azam na Ruvu JKT itakayochezwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam. Kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa sh. 1,000 kwa mzunguko na sh. 5,000 jukwaa kuu.
Wakati huo huo; SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Alfred Kisongole Lwiza kuwa Kamishna wa mechi ya Ligi ya Mabingwa (CL) kati ya El Merreikh ya Sudan na FC Platinum ya Zimbabwe.
Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza itachezwa Aprili 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa El Merreikh jijini Khartoum, Sudan kuanzia saa 2 kamili usiku. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa wikiendi hii jijini Harare timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
El Merreikh ni moja ya timu ambazo CAF iliziingiza moja kwa moja katika raundi ya kwanza. FC Platinum iliingia raundi ya kwanza baada ya kuing’oa Green Mamba ya Swaziland katika raundi ya awali.