TIMU za Simba na Yanga sasa zitaanza kuutumia Uwanja wa Azam Chamazi ulioko Mbande, Dar es Salaam wiki hii. Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema, Septemba 14 mwaka huu Simba itakuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma wakati siku inayofuata African Lyon itakuwa mwenyeji wa Yanga.
Aliongeza kuwa viingilio kwa mechi zinazohusisha timu za Yanga na Simba kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 7,000 tu vitakuwa sh. 15,000 kwa jukwaa kuu na sh. 5,000 mzunguko. Kwa timu nyingine za Dar es Salaam zinazotumia uwanja huo kiingilio kitaendelea kuwa kile kile cha sh. 10,000 jukwaa kuu na sh. 3,000 mzunguko.
Wakati huo huo, akizungumzia mapato kati ya Simba na Azam alisema katika mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa Septemba 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam alibainisha kuwa imeingiza sh. 72,167,000.
“Watazamaji waliokata tiketi kwa ajili ya kushuhudia mechi hiyo walikuwa 21,129. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 15,000, sh. 7,000, sh. 5,000 na sh. 3,000. Viti vya bluu na kijani ambavyo kiingilio kilikuwa sh. 3,000 viliingiza watazamaji 18,586, hivyo kuingiza sh. 55,758,000,” amesema Wambura.