MAHASIMU wa jadi timu za mpira wa miguu za Simba na Yanga zote za Dar es Salaam, zinatarajia kukutana tena Agosti 13, 2011 mchezo utakaochezwa katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mchezo huo utakuwa ni wa ufunguzi wa kuzindua msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom, inayotarajia kuanza rasmi Agosti 20, 2011.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa mtandao wa Thehabari kutoka TFF na Ofisa Habari wa Shirikisho hilo, Boniface Wambura jana jijini Dar es Salaam, jumla ya vilabu 14 vinatarajia kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom ambazo zimewasilisha usajili wa wachezaji wao kwa ajili ya ligi hiyo.
Mechi ya kuzindua msimu kati ya Simba na Yanga itachezwa Agosti 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Muda wa mwisho kuwasilisha usajili ilikuwa saa 6.00 usiku Julai 20 mwaka huu. Klabu zote ziliwasilisha usajili wao Julai 20 mwaka huu kwa wakati na muda waliowasilisha ukiwa ndani ya mabano.
Klabu hizo ni Ruvu JKT Stars (saa 9.00 alasiri), Oljoro JKT (saa 9.00 alasiri), Kagera Sugar (saa 9.00 alasiri), Ruvu Shooting (saa 10.00 jioni), Polisi Dodoma (saa 10.30 jioni), Moro United (saa 10.45 jioni), Simba (saa 1.30 usiku), Azam (saa 3.45 usiku), African Lyon (saa 4.30 usiku), Yanga (saa 4.30 usiku), Villa Squad (saa 5.30 usiku), Mtibwa Sugar (saa 5.40 usiku), Toto African (saa 5.50 usiku) na Coastal Union (saa 5.58 usiku).
Wakati huo huo, Daring Club Motema Pembe (DCMP) ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kupitia Shirikisho la vyama vya mpira wa miguu vya nchi hiyo (FECOFA) limetuma TFF maombi ya Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mshambuliaji wa Simba, Musa Hassan Mgosi.
Klabu hiyo imemuombea Mgosi hati hiyo ya uhamisho kama mchezaji wa ridhaa kwa maelezo kuwa imeshakubaliana na wenzao wa Simba katika suala hilo. Hivyo hivi sasa TFF inafanya mawasiliano na Simba kabla ya kufikia uamuzi wa kutoa ITC kwa DCMP.