Simba, Yanga kuchangia wahanga wa mafuriko

Baadhi ya wachezaji wa timu ya Yanga

KLABU za Yanga na Simba zitacheza mechi za kimataifa za kirafiki na mabingwa wa Malawi, Escom United siku ya Jumatatu na Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kuchangia watu waliokumbwa na janga la mafuriko jijini Dar es Salaam.

Kwa siku tatu mfululizo sasa mvua kubwa zimekuwa zikinyesha jijini Dar es Salaam na kusababisha baadhi ya watu kufariki, wengine kupoteza viungo na mali zao na hata watu kushindwa kufanya shughuli zao za kila siku.

Mratibu wa michezo hiyo kutoka kampuni ya Cute Youth Soccer Academy, Salum Mkemi alisema kupitia taarifa yake aliyosambaza kwenye vyombo vya habari kwamba mechi hizo zilizokuwa zifanyike kesho na kesho kutwa kwenye Uwanja wa Taifa zimesogezwa mbele kwa hiyo mechi baina ya Yanga na Escom sasa itachezwa Desemba 26 wakati ile ya Simba na Escom itakuwa Desemba 27.

Baadhi ya wachezaji wa Simba


“Nichukue fursa hii kutangaza kusogezwa mbele kwa mechi za kirafiki kati ya Yanga na Escom iliyokuwa ifanyike keshokutwa (kesho) pamoja na Simba na Escom iliyokuwa ifanyike Jumapili.

“Badala yake ule wa Yanga na Escom sasa utafanyika Desemba 26 na ule wa Simba na Escom utafanyika Desemba 27, sababu kuu iliyosababisha mabadiliko haya ni janga la mafuriko lililowakumba wananchi wenzetu ambao baadhi wamefariki, wengine wamepoteza viungo na mali zao,”alisema Mkemi.

Alisema,”Michezo hii haitakuwa burudani wala maandalizi ya michuano ya kimataifa isipokuwa itakuwa michezo ya kuchangia wahanga wa janga la mafuriko.”

Mkemi alisema kuwa kila tiketi itakayouzwa katika mechi hizo itakatwa Sh 500 ambayo itaingia moja kwa moja katika mfuko wa maafa mkoa wa Dar es Salaam.”Tunayaomba makampuni yajitokeze kudhamini michezo hii, sasa tushikamane, tuungane katika kipindi hiki kigumu,”alisema Mkemi.

Wakati huohuo; Mgogoro wa kimaslahi kati ya Kampuni ya Future Century na klabu ya Simba umesababisha kufutwa kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Gor Mahia dhidi ya Simba.

Future Century ambao ndio walikuwa waandaji wa pambano hilo walikuwa tayari kutoa asilimia 20 ya mapato yatakayopatikana katika mechi hiyo na kuipa Simba, lakini Wekundu hao wamekataa na kudai wapatiwe shs 25 mil. Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki ulikuwa umeandaliwa na Kampuni ya Future Century yenye maskani yake jijini Nairobi, Kenya na ulipangwa kuchezwa Januari Mosi ikiwa ni harakati za timu zote mbili kujiandaa na mechi za kimataifa za CAF na Ligi Kuu.

Kwa mujibu wa ofisa wa Future Century, Martha Enock alisema wameamua kufuta mchezo huo wa Simba dhidi ya Gor Mahia baada ya Simba kukataa dau lao la asilimia 20 la mapato ya mlangoni na kutaka kulipwa shilingi 25mil.

“Sisi tulitaka kuwapa asilimia 20 ya mapato yatakayopatikana siku ya mechi, lakini wao wamekataa wanataka tuwape shs 25mil, tumekaa na kujadili suala hili tumeona haitawezekana hivyo tumeamua kuifuta mechi hiyo ya Simba na Gor Mahia,”alisema Enock.

Katika taarifa yake kwenda kwa Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, ofisa huyo wa Future Century alisema kampuni yake haitaweza kumudu kiasi hicho cha fedha ilichohitaji Simba hivyo wameamua kuachana na mpango wa kuandaa mechi hiyo.

“Baada ya kujadili ada ya Simba waliyotaka, tumegundua hatutaweza kumudu gharama hizo, hivyo tumeamua kufuta mwaliko wa Simba kucheza na Gor Mahia mechi ya kirafiki ya kimataifa, nawatakia sikukuu njema ya X – Mass na Mwaka mpya,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Enock kwenda kwa Katibu wa Simba.

Jitihada za kuwatafuta viongozi wa Simba kulizungumzia suala hilo zilishindikana baada ya kutopatikana kwa njia ya simu ya kiganjani.Simba itaanza harakati zake za kucheza mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF kwa kucheza na Kiyovu ya Rwanda, wakati Gor Mahia itavaana na Ferroviario de Maputo ya Msumbiji, mechi za kwanza zitachezwa kati ya Februari 17 au 19 kabla kurudiana Machi 2 au 4.
CHANZO: Mwananchi