Simba yaifuata Yanga Taifa


Uwanja wa Taifa unavyoonekana kwa nje.

KLABU ya Simba imefuata nyayo za watani wao wa jadi Yanga, baada ya kuamua kuomba Uwanja wa Taifa kama uwanja wao wa nyumbani katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba imesema ina matarajio makubwa ya kutumia Uwanja wa Taifa kwa kuwa imeshapeleka maombi yao kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekeil Kamwaga alisema kuwa imeshapeleka maombi ya kutumia uwanja huo, hivyo wanachosubiri sasa ni kikao cha viongozi wa Serikali pamoja na TFF kuhusu matumizi ya uwanja huo.

“Tumeshawasilisha barua TFF nasi tumeomba kutumia uwanja wa Taifa kama uwanja wetu wa nyumbani, tuna matarajio makubwa ya kutumia uwanja huo, tunachosubiri sasa ni lini Serikali, TFF na viongozi wetu watakaa kuzungumzia matumizi ya uwanja huo,” alisema Kamwaga.

Ligi Kuu Tanzania Bara itaanza kutimua vumbi mwezi ujao, ambapo kabla ya kuanza kwa michuano hiyo kutakuwa na ufunguzi wake kwa kupigwa kwa mchezo wa Ngao ya Hisani,ambapo Simba na Yanga zitachuana Septemba 13 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Aidha, Kamwaga alisema kikosi chao kesho kitaanza mazoezi yake kwa ajili ya mashindano ya siku ya Simba (Simba Day) pamoja Ligi Kuu na Ngao ya Hisani.
Chanzo; Jambo Leo