Simba wakatiliwa kuwatumia Samata na Ochan

Taarifa hii ni kwa mujibu wa Boniface Wambura, Ofisa Habari wa TFF

Wachezaji Mbwana Samata na Patrick Ochan ambao Simba ilitaka kuwatumia kwenye
mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco hawana
uhalali wa kuchezea timu hiyo.

Simba kupitia TFF ilitaka kufahamu kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)
kama inaweza kuwatumia wachezaji hao kwa vile Hati ya Uhamisho wa Kimataifa
(ITC) kuichezea TP Mazembe bado haijatolewa.

Kwa mujibu wa CAF, hawawezi kuichezea Simba kwa vile tayari wameuzwa, hivyo
kutokuwa na sifa ya kuwa wachezaji wa timu hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 26 (1) ya
Kanuni za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sifa ya mchezaji kwa mujibu wa kanuni hiyo ni kuwa na leseni iliyotolewa na
chama cha mpira wa miguu cha nchi yake, leseni ya CAF, awe anaichezea timu
inayoshiriki Ligi ya Mabingwa kwenye ligi ya nchi husika na awe anaishi katika
nchi ilipo timu anayoichezea.