Timu ya Wekundu wa Msimbazi Simba Sc wameunguruma Mkoani Morogoro kwa kuitungua timu ya Burkina Faso kwa bao 3-0 kwenye mchezo wa Azam Sports Federation Cup (FA) mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Hamis Kiiza ametupia bao mbili kwenye mchezo huo wa jana, Kiiza alizama wavuni dakika ya 77 na kuipa Simba bao la kuongoza kabla ya kukwamisha tena bao lake la pili dakika ya 90 ambalo lilikuwa ni la tatu kwenye mchezo huo.
Goli jingine la Simba lilifungwa na Said Ndemla akiungana na Kiiza kuipa Simba ushindi kwenye mechi ya ugenini.Matokeo hayo yanaifanya Simba kusonga mbele kwenye hatua ya raundi ya nne ya mashindano hayo.
leo Jumapili michuano hiyo itaendelea kwa michezo mitatu, jijini Dar es salaam Young Africans watawakaribisha Friends Rangers uwanja wa Taifa, Njombe Mji watakua wenyeji wa Tanzania Prisons uwanja wa Amani Njombe, huku Stand United wakicheza dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Michuano hiyo itaendelea kesho Jumatatu, Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa Rhino Rangers katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Panone FC dhidi ya Madini FC uwanja wa Ushirika mjini Moshi na Africa Lyon wakiwa wenyeji wa Azam FC uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.
Matokeo ya mechi zote za leo michuano ya FA :
(Jamhuri, Morogoro) Burkina Faso 0-3 Simba SC
(Nagwanda, Mtwara) Ndanda FC 5-0 Mshikamano
(CCM Kirumba, Mwanza) Pamba 1-4 Toto Africans
Ratiba ya michezo ya kesho:
(Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam) Yanga SC vs Friends Rangers
(Amaan, Njombe) Njombe Mji Vs Prisons
(CCM Kambarage, Shinyanga) Stand Untd Vs Mwadui FC