Simba SC Yaanza Kuota Jiwe la Moto

MASHABIKI-SIMBA

SIMBA SC imelazimishwa sare ya bila kufungana na JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Selemani Kinugani wa Morogoro, aliyesaidiwa na Josephat Bulali wa Tanga na Omar Juma wa Dodoma, timu zote zilishambuliana kwa zamu.

Dakika ya saba mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Frederick Blagnon alipewa pasi nzuri na kiungo Jamal Mnyate, lakini shuti lake likadakwa na kipa wa JKT, Said Kipao.

Dakika ya 19 winga wa Simba Shizza Kichuya alipiga shuti kali na Kipao akapangua kabla ya JKT kujibu dakika ya 18 baada ya shuti kali la Saad Kipanga kufuatia pasi ya Atupele Green na kipa Vincent Angban.

Simba SC ilipata pigo dakika ya 73, baada ya beki wake Novat Lufunga kuumia mkono na nafasi yake kuchukuliwa na Juuko Murshid.
Kuingia kwa Mwinyi Kazimoto aliyechukua nafasi ya Jamal Mnyate na Ibrahim Hajib aliyechukua nafasi ya Blagnon kuliongeza kasi ya mashambulizi ya Simba, lakini sifa zimuendee kipa Said Kipao aliyeokoa michomo kadhaa ya hatari.

Kwa matokeo hayo, Simba inaangukia nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake nne, sawa na Azam FC wanaoongoza kwa wastani mzuri wa mabao.

Matokeo ya mechi nyingine zilizochezwa leo kwenye viwanja vingine:
Mtibwa Sugar 2-0 Ndanda FC
Azam FC 3-1 Majimaji FC
Tanzania Prisons 1-1 Ruvu Shootings
Mbao FC 0-1 Mwadui FC
Kagera Sugar 0-0 Stand United

Chanzo:www.binzubeiry.co.tz/