Simba na Yanga sasa kuvaana usiku Agosti 17

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo katika ofisi za shirikisho hilo Dar es Salaam (Picha na Joachim Mushi)

MECHI ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom kati ya mabingwa watetezi Yanga na Makamu Bingwa Simba itachezwa usiku (Agosti 17 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Dar es Salaam na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, uamuzi wa mechi hiyo kuchezwa usiku kuanzia saa 2.00 umetokana na sababu kadhaa, kubwa zikiwa ni Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na pia Agosti 17 mwaka huu kuwa ni siku ya kazi.

Wambura alisema pambano hilo litatanguliwa na mechi ya vikosi vya pili (U20) vya timu hizo ambayo yenyewe itaanza saa 10.30 jioni. Mechi ya Ngao ya Jamii baada ya dakika 90 kama mshindi hatapatikana, zitaongezwa dakika 30. Katika muda huo nao kama mshindi atakuwa bado hajapatikana, itatumika mikwaju ya penalti.

Aliongeza mechi hiyo imepata mwekezaji (Bigbon) na hivi sasa wadau wake wakuu- Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu husika ziko katika mazungumzo ya mwisho mwekezaji huyo. Kwa redio ambazo zinataka kutangaza mechi hiyo moja kwa moja zinatakiwa kuwasiliana na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TFF ili kupewa masharti ya kufanya hivyo.

Pia unafanyika utaratibu wa kuuzwa futari uwanjani mara baada ya mechi ya vikosi vya pili ili kuwawezesha washabiki waliofunga kutohangaika kutafuta sehemu ya kufuturu.