Simba, Mtibwa Waingiza Mil 102, Mjini Magharibi Copa Coca-Cola

Baadhi ya wachezaji wa Simba SC wakishangilia

MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Mtibwa Sugar iliyochezwa Septemba 14 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 95,080,000.
 
Watazamaji 16,507 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 15 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
 
Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 23,018,077.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 14,503,728.81.
 
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 11,704,107.18, tiketi sh. 2,548,890, gharama za mechi sh. 7,022,464.31, Kamati ya Ligi sh. 7,022,464.31, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,511,232.15 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,730,958.34.
 
MJINI MAGHARIBI MABINGWA COPA COCA-COLA
Mjini Magharibi imetwaa ubingwa wa michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 upande wa wavulana baada ya jana (Septemba 14 mwaka huu) kuifunga Ilala bao 1-0.
 
Mechi hiyo ya fainali ilichezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam. Ilala iliwavua ubingwa Morogoro baada ya kuwafunga kwenye mechi ya nusu fainali kwa kuivua ubingwa Morogoro katika mechi iliyoamriwa kwa mikwaju ya penalti.
 
Kwa upande wa wasichana, Mwanza ndiyo imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwa njia ya penalti dhidi ya Ilala. Hadi muda wa kawaida wa mchezo huo uliochezwa jana (Septemba 14 mwaka huu) jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam timu hizo zilikuwa suluhu.
 
*Imeandaliwa na Boniface Wambura Mgoyo, Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)