Simba kuanza Ligi Kuu Bara Leo

Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Simba

MICHUANO ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara inataraji kuanza leo huku Mabingwa watetezi Simba wakitarajiwa kuwakaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Wakati timu ya Simba ikitupa karata yake ya kwanza ya ligi hiyo timu zote 14 zitakuwa kwenye viwanja saba tofauti.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema; mjini Morogoro, Polisi Dodoma watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati jijini Tanga, Mgambo JKT ambayo imepanda daraja msimu huu itaumana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Tanzania Prisons ambayo nayo imerejea VPL msimu huu itaialika Yanga kwenye Uwanja wa Kumbukumbu
ya Sokoine jijini Mbeya. JKT Ruvu na Ruvu Shooting zitapambana kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam huku Azam ikiwatembelea Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Katiba.

Ofisa Habari huyo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania aliongeza Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans dhidi ya Oljoro JKT. Mechi zote zitaanza saa 10.30 jioni.

Boniface Wambura alisema Viingilio katika mechi ya Simba na African Lyon vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Viingilio kwa mechi nyingine vitakuwa sh. 3,000 na sh. 10,000.