SIKU ya Wapendao si Sikuu Rasmi nchini Marekani. Watu huenda kazini kama kawaida, hata hivyo kama zilivyo Siku Kuu nyingi nchini humu, nayo pia imekumbwa na kimbunga cha biashara tangu pale kampuni ya Hallmark ilipoanzisha kuzalisha kadi zao kwa wingi. Hii ni siku ya pili kwa wingi wa mauzo katika mwaka baada ya siku ya Christmas.
Inakadiriwa kuwa mauzo ya kadi hizo katika siku ya wapendanao ni zaidi ya dola billioni 15. Baadhi ya watani wanasema kuwa “iwapo sherehe za siku ya Wapendanao zitapigwa marufuku nchini Marekani, basi shirika la Hallmark litafilisika”
Biashara nyingine inayochangamka katika siku hii ni ya maua. Tani za maua huuzwa katika siku hii, na baadhi ya wauza-maua huajiri wafanyazi wa kiasi wiki moja kabla ya siku hii ili kukabiliana na ongezeko la wateja. Waridi ni nembo ya pili maarufu katika siku hii baada ya ile ya moyo.
Mbali na biashara hizo mbili, kuna zawadi aina kwa aina ambazo watu huwanunulia wale wawapendao, zikiwemo pipi, chakileti, na vitu vyengine vya kula na kunywa ambavyo ama hutengenezwa katika umbo la “moyo” kama ishara ya mapenzi, au kufungwa katika vifurushi vilivyopambwa katika mfumo kama huo.
Siyo Hallmark tu wanaofaidika katika siku hii, bali biashara nyingi mauzo yao huongezeka khususan mikahawa ambayo watu wanaotaka kudhirisha mapenzi kwa wapenzi wao hujazana katika sehemu hizo na kudhihirisha mapenzi ya hali ya juu kwa kuagizisha milo ya fakhari.
Kwa ujumla Waswahili wanasema “Mtu hujikuna ajipatapo”. Kwa hivyo, kuna wale ambao huwanunulia wapenzi zawadi khafifu kama vile kadi yenye thamani ya chini, na kendelea mpaka kufikia vito vya thamani, magari, majumba na sema upendavyo. Nchini Marekani, Canada na kwengineko, baadhi ya maskuli huandaa tafrija maalum za Siku ya Wapendanao ambapo wanafunzi hubadilishana zawadi na marafiki zao ambazo aghlabu huwa ni pipi, chakileti na kadi za maamkizi.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia siku hii wanasema kuwa; Wanaosherehekea na Wasiosherehekea siku ya wapendanao huzalisha mabilioni ya Dola nchini Marekani, hata hivyo wako watu ambao hawasherehekei siku hii kutokana na sababu mbalimbali. Wale wanaosherehekea wanaona kuwa ni siku iliyojaa upendo. “Siku ya Wapendanao ni siku iliyojaa upendo, anga yote huwa imejaa mapenzi”, anasema Angie Bradlye, Msimamizi wa Uzalishaji katika kiwanda kimoja nchini Marekani, na kuongeza, “ingawa mume wangu amefariki, lakini katika siku hii hujihisi kama niko pamoja naye na moyo wangu hujaa furaha. Anaona kuwa ni fursa kwa wanaume kudhihirisha mapenzi kwa wapendanao. “Ni siku muhimu kwa wanaume kudhihirisha mapenzi kwa wanawake wawapendao” alisema.
Kwa upande wa wale wasiosherehekea siku hii nao pia wana sababu zao. Scotty ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika na anasema “Mimi siadhimishi siku hii kwa sababu ni siku kuu iliyotengenezwa na Wazungu tu kwa ajili ya kujipatia pesa kutokana na mauzo ya biashara zao”
Hata hivyo, Blue, ni mwanamke wa Kizungu, lakini hasherehekei siku hii akisema “Huu ni upuuzi mtupu, si chengine chochote ispokuwa wanawake wasiokuwa na shukurani kujipatia zawadi wasizostahiki kutoka kwa mabwana zao”
Wengine huwa hawasherehekei kwa sababu hawana wapenzi wa kusherehekea nao, kama ambavyo Kendra Simpson kutoka Jimbo la Karolina Ya Kusini aliiambia Swahillivilla : “Mimi sisherehekei kwa sababu sina mpenzi kwa sasa, kama nina mpenzi na anapenda kuadhimisha siku hii, basi nitaingia naye pumbaoni”.
Hata hivyo alisisitiza kuwa kila siku inapaswa kuwa siku ya mapenzi kwa wapendao, na siyo siku hii moja tu. Rai hiyo inaungwa mkono na Bi LaToya Bragg wa jimbo la Ohio, ambaye anasema “ni jambo la kushangaza kuona watu wanahemkwa na kupoteza mapesa katika siku hii moja, wakati ambapo mapenzi yanatakiwa kudumu kwa muda wote ambao watu wapendanao huwa pamoja katika uhai wao”
Athari mbaya za Kijamii.
Bi. LaToya aliyeandika kitabu kwa jina “The Heart Of Me” pia haoni sababu ya kuadhimisha siku hii katika mfumo wake wa sasa kwa vile unaleta athari mbaya za kijamii. “Kuna watu wengine hali zao za kiuchumi siyo nzuri, kwa hivyo hawawezi kunnuua zawadi kwa wapenzi wao, na hivyo wapenzi wanaokosa zawadi kutoka kwa wapenzi wao, hujihisi duni mbele ya wenzao”
“Aidha huleta athari za kiuchumi kwa watu wenye kipato cha chini kwa kujikalifisha kuwanunulia wapenzi wao zawadi wazipendazo ambazo wakati mwingine ziko nje ya uwezo wao.
Lakini hufanya hivi ili tu na wao waonekani ni watu katika jamii”
Mbali na umaarufu wa siku hii, hata hivyo uchunguzi mdogo uliofanywa na Swahilivilla umeonesha kuwa, idadi kubwa ya watu hawajui asili, chimbuko na maana ya Siku ya Wapendanao. Kristy, ni afisa wa mapokezi na usafirishaji katika Shirika moja la vifaa vya magari anasema: “Ninavyojua siku hii ni ya wanaume kuwanunulia zawadi wapenzi wao, na kwa wanaume siku yao ni ile inayoitwa ‘sweetest hearts day’..”
Naye Amanda Waleker anasema: “Sijui chochote kuhusu asili ya siku hii, watu wanasherehekea na kuadhimisha, lakini mimi si katika mambo yangu”
CHANZO; Swahillivilla Blog