Chama Cha Watu Wenye Ualbino Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi za Watu Wenye Ulemavu, mashirika mengine yasiyo ya kiserikali na wadau mbalimbali mwaka huu watafanya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uelewa Juu ya Ualbino mjini Dodoma ambayo kilele chake ni tarehe 13 Juni.
Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni Takwimu na Tafiti kwa Ustawi wa Watu Wenye Ualbino. Maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuibua mijadala na tafakuri juu ya ukusanyaji endelevu wa takwimu, uchambuzi wake na upatikanaji wake kwa wakati kwa wadau.
Hii ni kwa mujibu wa wa Sheria namba 9 ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 pia kama ilivyo katika Ibara ya 8 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu, kwamba serikali inao wajibu wa wa kuwasajili na kuwahudumia na kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanakuwa salama lakini pia wajibu wa kukusanya takwimu zipatikane kwa watu wenye ulemavu na wadau wengine.
Kauli mbiu ya mwaka huu imezingatia uhalisia wa ukosefu mkubwa wa takwimu za watu wenye ualbino hapa nchini, hususan katika wakati huu ambao Taifa linatekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa mujibu wa Ajenda ya kimataifa 2030 ikiongozwa na kaulimbiu ya hataachwa mtu nyuma (no one will be left behind). Bila ya takwimu, hasa bila ya kuwa na utaratibu mzuri wa upatikanaji takwimu serikali haitaweza kupanga vyema juu ya ustawi wa watu wenye ualbino.
Takwimu ni suala la kitaifa na maadhimisho ya mwaka huu yanaibua mjadala wa takwimu kwa kutambua umuhimu mkubwa na jukumu kubwa la Ofisi ya Taifa ya Takwimu, hususan wakati ambao tunazo sheria mbili ambazo zina changamoto zake kwa makundi ambayo upatikanaji wa takwimu haujapewa kipaumbele:- 1. Sheria ya Takwimu Na. 9 ya mwaka 2015 ambayo imeanza kutumika rasmi tarehe 2/11/2015 kupitia tangazo la serikali Na. 491 la tarehe 30/10/2015. Pamoja na mambo mengi mazuri yaliyo kwenye sheria hii, ikiwemo nia njema ya kupata takwimu sahihi na zilizothibitishwa, inaweka zuio na adhabu kwa kuchapisha taarifa bila idhini ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Hii ni changamoto kubwa kwa wadau mbalimbali, wakiwemo watafiti na waandishi wa habari ambao wangesaidia katika upatikanaji wa takwimu mbalimbali. 2. Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 (The Cybercrimes Act, 2015) ambayo ni sheria nzuri sana, hususan kipindi hiki ambacho matumizi ya TEHAMA yanaongezeka kwa 1 kasi, hivyo umuhimu mkubwa wa dhahiri kudhibiti uchapishaji na usambazaji wa taarifa zisizo sahihi na zile za uchochezi, ambao hata sisi ni wahanga, lakini nayo ina changamoto kubwa hata kwa watunga sheria wenyewe nasi wadau wengine. Wakati sheria hizi mbili hazijafahamika vyema miongoni mwa wadau wengi mijini na vijijini, maadhimisho haya yanakusudia kuongeza ufahamu juu ya sheria hizi mbili na zaidi kutafakuri njia bora za kupata takwimu za kitaifa kwa watu wenye ualbino.
Tunatarajia kupitia maadhimisho haya Ofisi ya Taifa ya Takwimu itaweka utaratibu (mechanism) wa ukusanyaji takwimu endelevu, uchambuzi na upatikanaji kwa wadau, hususan serikali ambayo kwa sasa tunaona mwamko mkubwa katika ngazi mbalimbali kupanga na kuweka kwenye bajeti mahitaji ya watu wenye ualbino, kuanzia ngazi za halmashauri. Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ilisaidia kujibu swali gumu la “kuna watu wangapi wenye ualbino nchini” ambapo ilibainika wapo 16,376 (wanaume 7,620 na wanawake 8,756).
Hii ilikuwa ni hatua kubwa sana katika Taifa letu, pengine ndiyo nchi pekee iliyojumuisha takwimu za watu wenye ualbino kwenye sensa ya kitaifa. Kwa bahati mbaya, ambayo ni changamoto kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, bado maswali mengi hayajibiki kwa watu wenye ualbino na kaya zao, mfano takwimu kwenye upatikanaji wa elimu, ajira na hali za kiuchumi, uapatikanaji wa huduma za kijamii, ikiwemo kinga na tiba ya saratani ya ngozi ambayo inaongoza kusababisha vifo katika umri mdogo kwa watu wenye ualbino. Je, kama idadi ni hiyo 16,376 ni kweli serikali imeshindwa kuwafikia wote kwa huduma stahiki? Kwa makadirio ya ongezeko la watu kwa kiwango cha asilimia 3 kuanzia mwaka 2013, hadi sasa Watu Wenye Ualbino wanakadiriwa kuwa 18,833 (wanaume 8,763 na wanawake 10,070). Pamoja na kulenga kuibua mjadala utakaojenga utaratibu mzuri wa upatikanaji wa Takwimu kwa Watu Wenye Ualbino, hususan wakati huu ambao tunatekeleza Ajenda 2030, Watu Wenye Ulemavu kwa ujumla wanayo shauku kubwa ya kumsikia Mhe. Waziri Mkuu.
Yapo mengi yamefanyika tangu Mhe. Dr. John Pombe Magufuli ahamishie masuala ya Watu Wenye Ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu, baada ya ombi letu la miaka mingi kwa serikali. Tuna kiu kubwa ya kupata taarifa mbalimbali(updates) toka kwa Waziri Mkuu, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, ili pia tuone jinsi gani sisi taasisi za Watu wenye ulemavu na wadau wengine tunawezaje kusaidia juhudi zake na Ofisi yake na Serikali kwa ujumlakwa kwa ustawi wa watu wenye ualbino na ulemavu mwingine kwa ujumla.
Maadhimisho haya yanalenga kuongeza hamasa kwa jamii kuulewa ualbino. Chama Chetu kupitia matawi yake kote nchini tutashirikiana serikali na wadau mbalimbali kutekeleza shughuli mbalimbali. Tunaendelea kutoa rai kwa Katibu Mkuu TAMISEMI kutoa maelekezo ngazi ya Mikoa na Wilaya ili Maafisa Ustawi wa Jamii na wadau wengine waweze kujiandaa na kuwafikia watu wenye ualibno hasa wale ambao wako vijijini kwa huduma mbalimbali, ikiwemo kushirikisha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutumia maadhimisho haya kupata takwimu mbalimbali ambazo ni muhimu sana. 2 Baadhi ya shughuli zilizopangwa kitaifakuanzia tarehe 9-13/6/2017 ni:-
1. Hamasa kupita vyombo vya habari,mihadhara, vipeperushi na mabango;
2. Hamasa kupitia sanaa, hususan bendi kongwe na mahiri ya Tanzania One Theater (TOT Plus) ambao watafanya matamasha Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma;
3. Ukusanyaji wa takwimu za watu wenye ualbino;
4. Uendeshaji wa kliniki za ngozi na macho na utoaji wa misaada ya kisheria hapa Dar es Salaam na Dodoma;
5. Mdahalo (kongamano) kwa siku moja mjini Dodoma tarehe 11/6/17.
6. Adhimisho siku ya kilele linalotarajiwa kufanyikia uwanja wa Jamhuri Dodoma tarehe 13/6/2017 Wageni mbalimbali watashiriki katika maadhimisho haya, wakiwemo wadau wetu toka Sweden, Uholanzi, Marekani, Canada, Uingereza, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo na mataifa mengine.
Maadhimisho haya chimbuko lake ni hapa nchini ambapo tumekuwa tukiadhimisha tangu mwaka 2006 kabla ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2014 kupitisha azimio kuwa Juni 13 iwe siku ya Uelewa Juu ya Ualbino Kimataifa.
Maadhimisho haya kwa Tanzania humulikwa sana kama dira kwa nchi nyingine hususan za Afrika. Yana ushawishi mkubwa na yamechangia sana mabadiliko juu ya masuala ya watu wenye ualbino Kimataifa. Tunawakaribisha wadau mbalimbali kuchangia kwa hali na mali kuyafanikisha. Wanaoadhimisha siku zao za kuzaliwa (birthdays), harusi na matukio mengine tunawakaribisha kuyatumia maadhimisho haya kuleta mabadiliko, hasa kuifikia jamii kwa elimu. Tunamkaribisha kila mdau kwa nafasi yake.
Kwa kuwa wakati huo utakuwa ni mwezi mtukufu wa Ramadhan, tunaomba ushirikiano wa wadau kuchangia futari, na shughuli mbalimbali zilizoainishwa kufanyika Ili maadhimisho haya yaweze kufana, kuwafikia, kuwagusa na kuwastawisha Watu Wenye Ualbino na makundi mbalimbali ya watu wenye mahitaji maalum. Juni 15, 2017
Nemes Colman Temba
Simu: 0767 874592 0784 874592
Email: nemestemba@tas.or.tz