SIKIKA inaipongeza Wizara ya Fedha na Uchumi kwa kuweka vitabu vya bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 kwenye tovuti yake kwa wakati muafaka. Uamuzi huu wa kuweka wazi taarifa za bajeti unawawezesha wananchi kushiriki na kufuatilia mjadala wa bajeti na kuishauri serikali pamoja na wabunge kujadili masuala mazito yanayogusa wananchi ambao
ni wapiga kura na walipa kodi.
Awali, hapakuwa na utaratibu maalum wa kupata vitabu vya bajeti ya serikali na kulikuwa na ucheleweshwaji wa kuvisambaza kwa umma. Kwa miaka kadhaa sasa, Sikika na asasi nyingine za kiraia hapa nchini imekuwa ikitoa wito kwa serikali kusambaza vitabu vya bajeti kwa kupitia mtandao pamoja na njia nyingine ambazo zingewezesha wananchi kuvipata kwa urahisi.
Tumefarijika kwamba hatimaye ushauri huu umetekelezwa kwa vitendo na serikali baada ya Wizara hiyo kuweka katika tovuti yake, (www.mof.go.tz) vitabu vya bajeti toleo namba 2, 3 na 4. Vitabu hivyo sasa vinapatikana vikielezea kiasi cha fedha ambacho serikali inatarajia kukusanya na kutumia katika taasisi mbalimbali za umma nchini.
Kutokana na umuhimu wa taarifa hizi za bajeti, Sikika inawahimiza wananchi kutumia fursa hii kutembelea tovuti ya Wizara hiyo, kuchunguza kwa makini masuala nyeti yanayogusa ustawi wa maisha yao na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Hata hivyo, ili kuimarisha dhana ya ushirikishaji wa wananchi katika maendeleo yao, serikali inapaswa kukuza mbinu za
upashanaji wa taarifa kwa:-
1. Kuviweka vitabu vya bajeti katika tovuti kwa kutumia mfumo rahisi. Kwa sasa, vitabu hivyo vimewekwa katika mfumo wa PDF; na hivyo kusababisha ugumu wa kuchambua taarifa hizo.
2. Kuweka katika tovuti yake toleo namba 1 la bajeti hiyo, ambalo linahusu makadirio ya mapato ili kuwawezesha wananchi kulinganisha kati ya makadirio ya mapato na matumizi yanayopendekezwa.
3. Kuchapisha mapema kabla ya Bunge kuanza mjadala ili kutoa nafasi kwa wapiga kura kuwashauri wabunge wao katika maeneo ya kipaumbele.
4. Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2012, ni asilimia 11 tu ya wa Tanzania wanaotumia mawasiliano ya mtandao wa intaneti. Hivyo ni muhimu kuhamasisha wananchi kutumia vitabu hivyo vya bajeti vilivyowekwa katika tovuti.
Serikali ina wajibu wa kuimarisha miundombinu ya upatikanaji wa intaneti (mtandao) kwenye maeneo ya pembezoni, hususani vijijini.
Bajeti inaweza tu kuhudumia wananchi wake endapo itakuwa imezingatia mahitaji yao. Kwa mantiki hiyo, Sikika inatoa wito kwa kila mwananchi kupaza sauti kwa kuwaelekeza wawakilishi wao bungeni kuhakikisha kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14 inapunguza matumizi ya serikali yasiyo ya lazima.
Kwa mfano, matumizi ya serikali katika bajeti inayopendekeza ya mwaka 2013/14 ni kama ifuatavyo:-
• Tshs.360 bilioni kwa ajili ya posho, ambayo ni ongezeko la 15% ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita wa 2012/2013;
• Tshs.163 bilioni kwa ajili ya usafiri, ambayo ni ongezeko la 11% ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita;
• Tshs.79 bilioni kwa ajili ya makongamano, ikiwa ni ongezeko la 20% ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita 2012/2013;
• Tshs.24 bilioni kwa ajili ya ukarimu, sawa na ongezeko la 19% ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita;
• Tshs.71 bilioni kwa ajili ya mafuta na vilainishi, sawa na ongezeko la 6% ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita wa 2012/2013;
• Tshs.18 bilioni kwa ajili ya kununulia magari, ambayo ni pungufu ya 10%
ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita wa 2012/2013.
Kwa ujumla, Tshs.714 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2013/2014. Haya ni matumizi ambayo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka licha ya lengo la serikali la kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima tangu mwaka 2010. Wakati Waziri wa Fedha akiwasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2013/2014 (13 Juni, 2013), wabunge wanapaswa kuichambua kwa makini bajeti hiyo na kuishauri serikali
kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Wabunge wahimize kuongezwa fedha katika maeneo yanayonufaisha wananchi moja kwa moja kama vile kwenye kuboresha afya, elimu, maji, barabara, na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi n.k.
Kwa mara nyingine, tunaipongeza Wizara ya Fedha kwa kuweka vitabu vya bajeti kwenye tovuti kwa wakati mwafaka! Huu uwe mfano kwa Wizara zingine.
Irene Kiria
MkurugenziMtendaji; Sikika, P.O. Box 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Fax: 2668015, Email:info@sikika.or.tz, Tovuti: www.sikika.or.tz