Sijiuzulu ng’o-Meya wa Jiji la Arusha

Meya wa Manispaa ya Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo.

Na Janeth Mushi, Arusha

MEYA wa Manispaa ya Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo amesema
hawezi kujiuzulu wadhifa wake huo na kukanusha vikali kwamba hajavamiwa na majambazi kama taarifa zilivyovumishwa na baadhi ya watu wanaodai alitishiwa kuuwawa alipovamiwa nyumbani kwake.

Ametoa kauli hiyo leo mjini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, akitolea ufafanuzi masuala mbalimbali ukiwemo uvumi huo. Amesema uvumi unaotolewa dhidi yake ni chuki za kisiasa, hivyo kusisitiza hana mpango wa kuachia Umeya.

Amesema kuwa wanaotaka yeye ajiuzulu wadhifa wake ni wasiopenda maendeleo na wanafanya hivyo sababu ya chuki za kisiasa, hivyo ataendelea kuitumikia jamii ili kuleta maendeleo.

Hata hivyo Meya huyo alibainisha kuwa uvumi huo umemsababishia usumbufu kwani ndugu zake wamekuwa wakisafiri toka maeneo mbalimbali nchini kumjulia hali na huku baadhi ya viongozi wakimpa pole nyakati tofauti.

Akizungumzia suala la muafaka wa madiwani wa CHADEMA na Chama Cha
Mapinduzi (CCM), alisema kuwa walifikia hatua hiyo kwa lengo la kuleta maendeleo baada ya kuamuwa kuweka itikadi za vyama vyao pembeni na kuadi kuwa hakuna aliyeshurutishwa kufikai hatua hiyo.

“Siasa tumeshamaliza kwani kwa sasa uchaguzi umekwisha tunatatua
changamoto za wakazi wa Jiji la Arusha ili kuweza kuchochea kasi ya
maendeleo katika Jiji letu,” alisema Lyimo.

Alisema kuwa isifike wakati siasa zikaingizwa kwenye mambo ya msingi
ya maendeleo na ndio maana suala hilo kwa sasa limeachwa kwenye
mkono wa sheria ili hatua za kisheria zichukuliwe.