Mwandishi Wetu
Kwimba
USIMAMIZI mbaya sheria za uhifadhi wa mazingira na shughuli za kila siku za kijamii ni sababu zinazochangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira katika ziwa Victoria.
Hayo yalisemwa na msimamizi wa mradi wa uhifadhi wa mazingira ya ziwa Victoria awamu ya pili (LVEMP II) wilayani Kwimba, Radhimina Mbilinyi kwenye maadhmisho ya siku ya mazingira duniani yaliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Malemve wilayani hapa.
Alisema vyanzo vikubwa vya uchafuzi wa mazingira ya Ziwa Victoria ni pamoja na idadi kubwa ya mifugo inayopita mara kwa mara kufuata maji na malisho, kilimo kisichofuata kingamaji, ukataji ovyo wa miti, uelewa mdogo wa jamii kuhusu athari za mmomonyoko wa udongo, uchimbaji mchanga na kokoto hasa katika mito inayopeleka maji katika ziwa Victoria.
Mbilinyi alisema madhumuni ya kutoa elimu katika maadhimisho hayo juu ya uhifadhi wa mazingira ya ziwa Victoria ni pamoja na kuwashirikisha wadau wa uhifadhi wa mazingira katika kutunga sheria za kulinda vyanzo vya maji, kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi, wanajamii kuwa na shughuli mbadala za kiuchumi katika maeneo karibu na mto Simiyu.
Mengine ni kuongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na wanyama, kuanzishwa kwa jumuiya za watumiaji maji pamoja na kusimamia na kutekeleza mpango wa Wilaya wa uhifadhi wa mazingira kwenye Dakio la Mto Simiyu kwa miaka mitatu kama ulivyoridhiwa na mkutano wa wadau wa mazingira uliofanyika Machi Wilayani hapa.
Kwa awamu ya kwanza ya mradi wa uhifadhi wa mazingira wa Ziwa Victoria na awamu ya pili ulionza mwaka 2009 hadi 2013 utashirikisha maeneo yenye mabonde ambayo yana uchafuzi mkubwa ambayo humwaga maji katika ziwa Victoria.
Katika uchunguzi wa LVEMP wamebaini mito mitatu ambayo inaonekana kuwa ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa ziwa Victoria ambayo ni Simiyu uliopo Tanzania, Katonga wa Kenya na Nyami wa Uganda.