Shivji amkosoa Kikwete kuhusu katiba

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji

MWENYEKITI wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere Profesa Issa Shivji amekosoa Sheria ya Mchakato wa Kuundwa kwa Katiba mpya iliyosainiwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni na kusema kuwa ni mbovu na haitazaa katiba bora.

Novemba 29 mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alitia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 huku kukiwa na malumbano makali kutoka asasi za kiraia, vikiwemo vyama vya siasa, kupinga hatua hiyo kwa maelezo kwamba, mchakato huo uliendeshwa kwa mizengwe na Hata hivyo, taarifa ya kusainiwa muswada huo iliyotolewa na Ikulu kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa hatua hiyo ya Rais Kikwete, ilikamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kupitisha muswada huo uliowasilishwa na Serikali huku ikiweka wazi kuwa Serikali itaendelea kusikiliza maoni na mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria hiyo.

“Mheshimiwa Rais Kikwete anatoa wito kwa mwananchi yeyote mwenye maoni ama mawazo ya namna ya kuboresha Sheria hiyo, ajisikie yuko huru kutoa maoni yake na Serikali itasilikiza na kuchukua hatua zipasazo’’ ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu Akizungumza katika kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa na kituo cha televisheni ya ITV juzi usiku, Profesa Shivji ambaye ni mmoja wa magwiji wa sheria hapa nchini, alisisitiza kuwa sheria hiyo ni mbovu na kamwe haitazaa katiba bora wanayoitaka wananchi na kuwashauri kwenda kupinga jambo hilo mahakamani.”

Akichambua sheria hiyo, Profesa Shivji alikosoa kifungu cha 21 akisema kuwa inashangaza kwani kinazuia hata watu kuikosoa sheria hiyo. “Mimi nasema kuwa sheria hii ni mbovu…Katika sheria hii, kifungu hiki kinanizuia hata kusema, sheria hii ni mbovu’. Mimi sijui kulikuwa na fikra gani kuweka kifungu kama hiki, kitu kimoja tu ni kwenda mahakamani kuipinga.” Alisema. 

Akichambua kifungu kimoja baada ya kingine katika sheria hiyo, Profesa Shivji alisema kuwa imewatenga kabisa wananchi katika mchakato mzima wa kuandikwa kwa katiba mpya. “Wananchi wanatakiwa kushirikishwa tangu hatua ya kwanza, kwa mchakato wa Bunge, yaani sisi wenyewe tumeshirikishwa kupitisha sheria hiyo kuhakikisha vyombo vyote vinavyohusika vinafuatwa.” Alisema Profesa Shivji.

Akitoa mfano wa Kamati ya Bunge ya Masuala ya Katiba, Profesa Shivji alisema kuwa, haikufanya kazi yake kikamilifu hivyo kuwanyima wananchi fursa ya kutoa maoni. “Tulianza awali lakini hatukukamilisha…hatukuwa na sababu ya kutokukamilisha. Tulipoanza kwenye makongamano yale yaliyofanyika tulipata maoni ya wananchi, baada ya kupata maoni, ndipo mchakato wa kuunda katiba,’’ alisema Tume ya Rais ya Katiba Kuhusu Tume ya Rais ya Kuunda Katiba, Profesa Shivji, alisema haipaswi kuwa moja kwa moja chini ya Rais bali pia ishirikishe wananchi. 



Alitoa mfano wa tume ya aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei iliyoshughulikia Marekebisho ya Fedha na Tume ya Rais ya Ardhi lakini akasema, Tume ya Katiba siyo ya rais, Hii siyo Tume ya Rais, ni Tume ya Katiba (Constitutional Commission), inayoundwa chini ya sheria zilizopitishwa na Bunge. Hata tume iliyounda Katiba ya mwaka 1977 iliundwa chini ya Mkataba wa Muungano.

Sheria ile ilitaja wazi kwamba rais akikubaliana na Rais wa Zanzibar, ataunda Tume ya Katiba” alisema. Aliendelea kusisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika tume hiyo akisema kuwa rais anapaswa kuzingatia maoni ya wananchi katika uteuzi wa wajumbe wake. “Mfano taasisi mbalimbali za jamii zetu, taasisi za serikali, vyombo vya habari, vyuo vikuu, wanaweza kupendekeza majina mawili, tunaona kwamba hawa watu wanafaa kuwa wajumbe, halafu rais anateua kupitia hayo. 

Hiyo ndiyo namna ya kuwashirikisha wananchi lakini kwa sheria ya sasa hatujui rais anatumia vigezo gani,” alisema.

Bunge la Katiba Kuhusu Bunge la Katiba, alisema idadi ya wajumbe 600 wa Bunge hilo ni kubwa mno ukilinganisha na idadi ya Watanzania 40 milioni, hali ambayo alisema italifanya Bunge hilo kutumia gharama kubwa bila sababu. Alitoa mfano wa Bunge lililounda katiba ya uhuru ya India la mwaka 1947 akisema lilikuwa na wajumbe 250 na wakati huo idadi ya wananchi wakiwa 100 milioni.

Alikosoa pia uwiano wa idadi ya wajumbe hao akisema kuwa kati yao, teluthi mbili, yaani wajumbe 400 watakuwa ni wa CCM. Akasema hali hiyo itawanyima fursa wananchi ambao si wanachama wa vyama vya siasa. Kura ya maoni Kwa mujibu wa Profesa Issa Shivji, japo wananchi watapata nafasi ya kupiga kura ya maoni, bado kuna hatari ya kutopata katiba bora kwani hawakupata nafasi ya kutosha ya kutoa maoni yao. 



“Katiba inaweza kuwa na ibara 500, inawezekana kati ya hizo hupendi ibara mbili tu. sasa ukisema hapana ndiyo umeikataa katiba yote kwasababu hatukufuata vizuri mchakato,” alisema na kuongeza; “Hata Hitler aliingia madarakani kwa kura ya maoni”. Aliongeza kuwa kuna hatari katiba ikapitishwa na idadi ndogo ya wananchi hasa kutokana na tabia ya wananchi kutopenda kupiga kura.

“Sheria hiyo inasema kuwa asilimia 50 ya waliopiga kura siyo waliojiandikisha. Unaweza kukuta katiba ikapitishwa na asilimia 20 tu ya wananchi”.



Mjadala huo pia uliwahusisha Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha UDP, Isaac Cheyo ambao pia waliipinga sheria hiyo. Kwa upande wake Mnyika alieleza sababu ya wabunge wa Chadema kususia mjadala wa katiba na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge akisema kuwa walipinga muswada huo kusomwa kwa mara ya pili. Alifafanua pia hatua ya chama hicho kwenda Ikulu kumwona rais akisema kuwa rais ni upande wa pili wa Bunge. Mnyika alisisitiza kuwa Chadema hawatasubiri kwenda mahakamani, ili kupinga sheria hiyo bali watafanya mikutano nchi zima na kueleza ubaya wa sheria hiyo.



“Tutakwenda kwa wananchi tuwaambie ubaya wa sheria hii. Watapiga kura ya hapana, hata kama hatutapata katiba, tutakuwa tumeleta mabadiliko”. Naye Cheyo alisema mchakato mzima wa kuandikwa kwa katiba mpya umehodhiwa na rais huku wananchi wakizuiwa kutoa maoni yao. “Bunge la kutunga katiba ni Bunge la chama kile kile, limekuwa likiaminiwa na chama hicho hicho.

Tuangalie ‘composition’(wanaounda) ya Bunge, inachukuwa watu gani, vinginevyo tutakuwa hatuwatendei haki wananchi,” alisema Cheyo. Awali asasi mbalimbali ndani ya jamii zikiongozwa na Jukwaa la Katiba Tanzania, zilieleza kutoridhishwa na hatua zilizochukuliwa na serikali katika kuendesha na kusimamia mchakato mzima wa kupitishwa kwa sheria hiyo.

Wanaharakati walitishia kuitisha maandamano endapo Bunge lingeipitisha sheria hiyo huku Chama Wanasheria Tanzania, kikitishia kufikisha suala hilo mahakamani. Hata hivyo tangu Rais Kikwete aliposaini sheria hiyo, amekuwa akikutana na makundi mbalimbali, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa na kupokea maoni ya kuhusu kutungwa kwa katiba mpya.

CHANZO: Mwananchi