Shirikisho la Kisiasa ni dawa sahihi ya mtangamano EAC-Dk Sezibera
Na Nicodemus Ikonko, EANA
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera amesema Shirikisho la Kisiasa ni dawa (penincilini) sahihi kwa utulivu na uimarishaji wa mtangamano wa kanda hiyo ya Afrika Mashariki.
‘’Shirikisho la Kisiasa ni dawa ya penicilini kwa utulivu na mtangamano imara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ningependa kumshukuru kwa dhati mama Kiraso (Beatrice) kwa kutufanya tuweze kunywa dozi sahihi ya dawa hiyo,’’ Dk. Sezibera aliwaambia wafanyakazi wa EAC na wageni waalikwa Jumapili katika sherehe fupi iliyoandaliwa kwa heshima ya kumuaga Naibu Katibu Mkuu wa EAC, Beatrice Kiraso ambaye amemaliza mkataba wake wa kazi.
Alifafanua kwamba katika kipindi cha miaka sita ya utumishi wake katika Jumuiya, Kiraso, maarufu kwa jina la ‘’Mama Federeation(Shirikisho)’’ aliweza kuweka msingi imara wa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.
Akizungumza katika ghafla hiyo Kiraso alisema, anafurahi kwamba anaondoka EAC wakati ambapo baadhi ya mambo ambayo yalionekana kuwa mwiko kuyaazungumza wakati anajiunga na EAC, sasa yanajadiliwa kwa uwazi na wana Afrika mashariki.
“Ilikuwa mwiko kuzungumzia rushwa, utawala bora na Shirikisho la Kisiasa, lakini hilo siyo tatizo tena sasa. Natumaini kwamba itifaki ya utawala bora siku moja itatiwa saini,” Kiraso alisema.
Aliwashukuru wafanyakazi wa wote wa EAC pamoja na uongozi kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chake cha miaka sita na kuwatakia mafanikio mema katika kazi zao za ujenzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ikiwa kama shukurani kwa mchango wa Kiraso katika Jumuiya hiyo, Sekretarieti ya EAC, itachapisha kitabu chenye kurasa 450 kinachohusu njia ya EAC kuelekea katika Shirikisho la Kisiasa.Kitabu hicho kilizinduliwa rasmi katika ghafla hiyo ya kumwaga Kiraso, iliyofanyika katika hoteli ya Arusha.
Kiraso anakwenda kufanyakazi kama Mkuu wa wa Taasisi ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, yenye makao yake makuu, Lusaka, Zambia.