Na MwandishiWetu
Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Hailemariam Desalegn amesema Shirika la Meli la Ethiopia (Ethiopian Shipping Line) lipotayari kuanza kuitumia Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kutoa huduma nzuri.
“Shirika letu la Meli ambalo ni la kihistoria na lililobaki pekee katika ukanda wa Afrika likiwa linamilikiwa na Serikali ya Ethiopia sasa lipotayari kufanya kazi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania,”amebainisha Desalegn.
Ameongeza kuwa mbali na shirika hilo la meli kuwa tayari kuanza kuleta meli zake Bandari ya Dar es Salaam pia Shirika Kongwe la Ndege la Ethiopia (Ethiopian Airline) lenye mafanikio makubwa nalo litaanza kusafirisha mizigo inayopitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine Desalegn amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Menejimenti ya TPA katika kuboresha huduma zake ambapo amesema jitihada hizo sio tu zitanufaisha Serikali zote mbili bali pia ustawi wa maisha ya watu wa Tanzania na Ethiopia nao utaimarika.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Kassim amemshukuru Waziri Mkuu wa Ethiopia kwa kuja nchini ambapo amemuahidi kwamba mahusiano mazuri ya liyopo baina ya nchi hizi mbili yatadumishwa kwa maslahi mapana ya mataifa yote.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa amesema TPA itaendelea na mipango iliyopo ya kuhakikisha inaboresha Bandari zake ili ziweze kuhudumia vyema wateja wote kwa wakati.
“Tutaendelea kuboresha huduma zetu za Bandari na za sekta ya uchukuzi kwa ujumla ili tuweze kufikia malengo yenu na wateja wetu ya kuhakikisha kwamba tun awahudumia vizuri na kwa ufanisi,” amesema Mbarawa.
Mapema akitoa taarifa ya utendaji wa Mamlaka, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alimweleza Waziri Mkuu wa Ethiopia kwamba kwasasa TPA inaendelea na mpango wake wakujenga uwezo wakuhudumia wateja wake kwakuzingatia kwamba sekta ya uchukuzi inakuwa kwa kasi.
“Kutokana na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi nchini na Duniani kwaujumla, TPA inaimarisha uwezo wake wakuhudumia mizigo na meli kubwa ili kujenga uwezo kabla ya mahitaji makubwa kujitokeza”, amesisitiza Mhandisi Kakoko.