Mafuta yatachukua muda kurejea hali yake-Ewura

Wananchi Dar es Salaam wakiwa kwenye foleni ya mafuta katika moja ya vituo.

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Mafuta na Maji (EWURA) imesema hali ya kawaida kwa upatikanaji wa nishati za mafuta hasa dizeli na petroli itachukua muda kabla ya kureje katika hali yake ya awali.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Ofisa Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo alipokuwa akihojiwa na chombo kimoja cha habari, kuelezea utekelezaji wa wamiliki wa vituo vya mafuta na waagizaji wa nishati hiyo, kufuatia amri ya saa 24 iliyotolewa na Serikali.

Alisema tayari kampuni mbili zilianza kuuza mafuta tangu jana ikiwa ni muda mfupi tangu kutolewa kwa amri hiyo, iliyozitaka kampuni za BP, Oilcom, Engen na Camel kutekeleza agizo la Serikali ndani saa 24, ikiwemo kuanza kuuza na kusambaza nishati hiyo, pamoja na kujieleza kwanini wasiadhibiwe kwa kero walioisababisha kwa wananchi.

Alisema hadi jana mchana majira ya saa saba tayari baadhi ya kampuni mbili zilikuwa zikiuza mafuta na kusambaza katika vituo vyao, hali ambayo ilionesha walikuwa wakitekeleza amri ya Serikali. Hata hivyo alisema hali ya kawaida itachukua muda kurejea kutokana na mlolongo wa taratibu za kawaida za upakuaji wa mafuta hayo kwenye vituo vya kuuzia.

“Baadhi ya makampuni yameanza kutii amri tulioitoa tangu jana…tumekuwa tukifuatilia na hadi sasa (jana mchana) tumeshuhudia mafuta yakiuzwa na kusambazwa vituo, lakini hali itaendelea kurejea kama ilivyokuwa awali taratibu…zipo taratibu zingine kama vile usambazaji wa mafuta haya kwenye vituo kabla ya kupakuwa lazima mafuta yatulie kisha kupimwa…hatua kama hizi zinachukua muda fulani,” alisema Kaguo.

Baadhi ya vituo vikiwa vimeendelea kufungwa kwa kisingizi cha kukosa nishati hiyo, licha ya amri ya kuwataka kutoa huduma hiyo ndani ya saa 24 tangu juzi jioni.


Alisema EWURA inaendelea kufuatilia ikiwa ni pamoja na kusubiri utekelezwaji wa hatua zingine zilizokuwa ndani ya maagizo yaliyotolewa na Serikali kupitia mamlaka hiyo. Jana baadhi ya vituo vilianza kuuza nishati hiyo licha ya vingine kuendelea na mgomo huo baridi.

Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu baadhi ya maeneo ulishuhudia foleni ndefu za watu na magari kuingia katika vituo hivyo, jambo ambalo lililazimika askari polisi kuingilia kusimamia uuzaji ili kuondoa vurugu.

Baadhi ya vituo vilionekana kuendelea kufungwa na vingine kudai vimeishiwa na nishati hiyo. Maeneo ya barabara ya Mandera polisi walilazimika kuzuia baadhi ya wananchi waliokuwa wakiandamana na kukagua vituo vya mafuta ili kujiridhisha kama kweli havina nishati hiyo, ambapo walitishia kuvichoma moto endapo wangelikuta vinafanya udanganyifu.

Barabarani idadi ya magari tangu asubuhi ya jana ilionekana kupungua, kwa kile magari mengi kuegeshwa kwa kukosa nishati hiyo. Baadhi ya watu walipata mwanya na kununua na kuuza kinyemela kwa bei ya juu zaidi.

Wafanyakazi katika moja ya vituo wakiwa wamepumzika na kupiga soga. Kituo hichi hadi jana mchana hakikuwa kikitoa huduma kwa madai kimeishiwa na nishati hiyo.