MBUNGE wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), sasa ni dhahiri kwamba haafikiani na mikakati ya chama hicho.
Wakati viongozi wakuu wa Chadema wakiungana na wabunge wa NCCR-Mageuzi kupinga posho za vikao, Shibuda si tu kwamba anataka ziendelee, bali ziongezwe kutoka Sh 70,000 hadi Sh 500,000 kwa siku.
Shibuda alitoa msimamo huo unaokinzana na wa chama chake alipokuwa akichangia makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012, jana.
“Kutofautiana kifikra siyo usaliti, bali ni utarartibu wa kawaida na nimeamua kuyasema haya kwani kila binadamu ana uwezo wake wa kufikiri.
“Atakayeshindwa kunielewa basi niko tayari kukaa naye na kumweleza nina maana gani katika haya nitakayoyasema na nini maana yake.
“Ukweli una tabia ya kuudhi mtu dhurumati, lakini ukweli utabakia kwamba mimi ndiye mgombea peke katika nchi hii niliyefanya kampeni kwa siku nne kosha harusi ikajibu.
“Hili suala la posho limekuwa likizungumzwa sana na watu, nataka niwaambie kuwa enzi za mkoloni posho ilikuwa ikiitwa ujira wa mwia, na namtaka Waziri wa Fedha ayachukue haya, tunaomba jina la posho liondolewe liwekwe hilo neno la mwia badala ya posho.
“Kwa hiyo naomba ujira wa mwia uongezwe wabunge tulipwe hata laki tano kwa sababu huu tunaolipwa hautoshi kabisa.
“Nayasema haya kwa sababu najua kutofautiana kifikra ni sawa na panadol extra, naomba nieleweke hivyo, wanaozikataa posho ni wabunge maslahi binafsi kwa sababu hao hawachangii misikiti, hawachangii sherehe, na sherehe zingine,” alisema Shibuda na kupigiwa makofi na wabunge wanaounga mkono utaratibu za posho za vikao.
Wakati mbunge huyo akiyasema hayo huku hotuba yake ikitawaliwa na misemo ya kila aina, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye alikuwapo bungeni, alioenakana kiwa aameshika tama.
Shibuda alipomaliza kuzungumza, Mbowe alicheka akionyesha kushangazwa na msimamo wa mwanachama huyo ambaye uanachama wake ndani ya Chadema ni wa nusu mwaka.
Katika hatua nyingine, Shibuda ambaye mara kwa mara amekuwa akitofautiana na msimamo wa chama chake, aliishutumu CCM kwa kusema kuwa alipokuwa ndani ya chama hicho hakujua hali livyo katika upinzani, lakini baada ya kuingia katika upinzani amejua mitazamo ya CCM kwa vyama vya upinzani.
‘Nilipokuwa CCM sikujua hali ilivyo katika upinzani, mengi sikuyajua kabisa, CCM mmenilea wenyewe, CCM mmnenifunza mengi sana kumbe ukiwa upinzani wewe unaambiwa ‘siyo mwenzetu’.
“Ukiwa upinzani ukizungumza na mkuu wa wilaya unaambiwa ‘huyo siyo mwenzetu’, ukiwa upinzani ukizungumza na OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) unamabiwa huyo si mwenzetu, kama hali ni hiyo basi ni bora tufute mfumo wa vyama vingi, tuufute hauna maana.
“Sitaki CCM ife, lakini ijue kwamba kujivua gamba siyo kuondoa kikwapa, bali kikwapa kinaondolewa kwa udi,” alisema.
Source: Mtanzania