Shibuda kufukuzwa!

Mbunge wa Maswa Magharibi(Chadema), Mh. John Shibuda

 

   Lissu asema wanajipanga uchaguzi mdogo
*Aandikiwa barua akitakiwa atoe maelezo
*Kamati Kuu Chadema kutoa msimamo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

HAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kipo tayari kuingia katika uchaguzi mdogo katika Jimbo la Maswa Magharibi iwapo Kamati Kuu itaamua kumvua uanachama Mbunge wa Jimbo hilo, John Shibuda (CHADEMA).

Msimamo huo ulitolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), jana.

Lissu alikuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya kutakiwa kutoa msimamo wa chama hicho kuhusu Shibuda.

“Hatutishiki na lolote, kama ni kuingia katika uchaguzi mdogo tutaingia kama itabidi kufanya hivyo, wala hakuna mashaka yoyote.

“Leo (jana) namwandikia barua ili ajieleze ni kwa nini ameamua kutofautiana na msimamo wa chama na kama yupo hii barua atakabidhiwa leo (jana), barua hii naiandika kwa kutumia hansard (taarifa rasmi ya Bunge) yenye maelezo yake aliyoyatoa siku ile kwa sababu sitaki kumwonea mtu.

“Hili suala halitaishia hapa, baadaye litapelekwa mbele ya Kamati Kuu ya chama kwa sababu yenyewe ndiyo yenye jukumu la kumchukulia hatua ikiwamo kumfukuza uanachama kwani sisi hatuwezi kumfukuza ila tunachoweza kufanya ni kumtenga miongoni mwetu.

“Katika hili nasema tuko tayari kwa lolote, kama yeye anasema CHADEMA ni mbaya anaweza kutafuta sehemu nyingine ya kwenda atakayoona inamfaa kuliko kuendelea kutuvuruga.

“Amekaririwa akisema CHADEMA ni mbaya, sasa yeye aendelee tu kutusema kwa sababu hana jipya, hana lolote huyo kwa sababu anachokieleza ni kama matapishi ya wale wa jana na juzi waliokuwa wakiisema vibaya Chadema kwamba ni chama cha familia ya Mtei (Edwin Mtei) na mke wake Mbowe.

“Watu wamesema sana, wengine walidiriki kusema CHADEMA ni chama cha Wachaga, ngoja aendelee kusema kwa sababu naamini hana jipya, hatazungumza nje ya waliyowahi kusema waliomtangulia,” alisema Lissu.

MTANZANIA ilipomtafuta Shjibuda kwa simu ili azungumzie kauli ya Lissu, hakupatikana.

Wakati Shibuda akichangia bungeni Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 bungeni mjini hapa, alitofautiana na msimamo wa chama chake wa kuwataka wabunge wa chama hicho kutopokea posho za vikao vya Bunge.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa ngazi za juu wa chama hicho, wamekaririwa kwa nyakati tofauti wakisema kuwa posho ya vikao vya wabunge ni haramu kwa kuwa wabunge wanapohudhuria vikao hivyo ni sehemu ya kazi zao.

Shibuda alipokuwa akichangia bajeti hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, aliliambia Bunge kuwa Serikali inatakiwa kuongeza posho za vikao vya Bunge kutoka Sh 70,000 wanazolipwa kwa sasa hadi Sh 500,000 ili wabunge waweze kufanya kazi zao kwa mafanikio zaidi.

Kwa mujibu wa Shibuda, uamuzi wa wabunge wa Chadema kukataa kulipwa posho haukuwa sahihi kwa sababu posho ndicho kipozeo cha wabunge masikini kama yeye ambao hawana biashara za kuendeshea majimbo yao.

Hata hivyo, wakati akizungumza na gazeti dada la MTANZANIA, MTANZANIA Jumapili wiki iliyopita, mbunge huyo aliwashutumu Mbowe na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Kabwe Zitto, kwamba wanahatarisha demokrasia ya chama hicho kwa kuwa wanakiendesha kama chombo chao binafsi.

Alisema kuwa pamoja na kwamba Zitto na Mbowe wanasema suala la kukataa posho ni msimamo wa chama, kauli hizo siyo sahihi kwa kuwa msimamo huo ni msimamo wa viongozi hao wawili ambao wamekuwa na kawaida ya kuwatisha wabunge wa chama hicho pindi wanapoonekana kupinga mawazo yao.

Source: Mtanzania