Maafisa wa Nigeria wametangaza sheria ya kutotoka nje katika mji wa Kaskazini Mashariki wa Damaturu kufuatia makabiliano makali kati ya jeshi na wapiganaji wa kisiilamu na pia sheria hiyo imerejeshwa tena katika jimbo la Kaduna.
Makabiliano kati ya jeshi na wapiganaji wa kiisilamu eneo la Damaturu yalianza Jumatatu, siku moja baada ya kutokea mashambulio ya mabomu yaliyolenga makanisa jimbo la Kaduna na kudaiwa kutekelezwa na kundi la Boko Haram.
Mashambulio ya Boko Haram yalisababisha vifo vya watu 16 na kuchochea machafuko ya kulipiza kisasi ambapo makumi ya watu waliuawa.
Ramani ya jimbo la Yobe
Afisa mmoja katika hospitali ya Damaturu ameambia shirika la habari la AFP kwamba usalama umezorota na imekuwa hatari kwa wafanyikazi kuondoka hospitalini.
Polisi wa Nigeria wamelaumu Boko Haram kwa kulenga vituo vyao na jeshi ambapo maafisa watano waliuawa eneo la Damaturu hapo Jumatatu.
Rubaa za karibuni zinasema milio ya risasi imepungua katika jimbo la Yobe. Hii ni kwa mujibu wa mkuu wa polisi jimbo hilo Patrick Egbuniwe.
Damaturu,ni makao makuu ya jimbo la Yobe ambalo , Magharibi mwa jimbo la Maiduguri na ngome kuu ya Boko Haram.
Jina la Boko Haram linamaanisha kwamba elimu ya kisasa ni haramu. Kundi hilo linashinikiza sheria ya kiislamu {Sharia} kutangazwa kote nchini Nigeria na limetekeleza mashambulio makali nchini humo.
-BBC