Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete leo ameongoza maelfu ya Watanzania wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na viongozi mbalimbali katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 48 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Sherehe za maadhimisho zilipambwa na gwaride lililoandaliwa na majeshi mbalimbali ya Tanzania pamoja na vikosi vyake, ambapo Rais Kikwete alikagua gwaride maalumu kabla ya kutoa heshima kwa kiongozi huyo mkuu wa nchi.
Aidha Rais Kikwete ametoa msamaa kwa wafungwa 2,923 ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya sherehe za miaka 48 ya muungano. Kwa mujibu wa taarifa yake iliyosainiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, Rais ametoa msamaa kwa wafungwa wanaotumikia kifungo cha muda mfupi.
Wafungwa waliosamehewa ni pamoja na wanawake wajawazito na wenye watoto wanaonyonya, wafungwa wenye matatizo ya akili, wenye ugonjwa wa Ukimwi. Taarifa hiyo imesema msamaha uliyotolewa hauwahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, vifungo vya maisha, wafungwa wa madawa ya kulevya.
Msamaha huo hauwahusu wafungwa wa makosa ya rushwa, wenye makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, wafungwa wa makosa ya kunajisi, kulawiti, kubaka na wizi wa magari kwa kutumia silaha, wafungwa waliopatikana na makosa ya kupatikana na silaha na risasi, wenye makosa ya kuwapa mimba wanafunzi wa sekondari na msingi walio na zaidi ya miaka 18.
Msamaha huo pia hauwahusu waliopatikana na makosa ya wizi wa nyaya za umeme na mafuta ya transfoma, wanaohukumiwa kifungo cha makosa ya kutumia vibaya madaraka yao, wafungwa waliowahi kutoroka chini ya ulinzi na wale wanaotumikia vifungo vya kuwazuia watoto wao wasipate masomo.