MECHI ya kirafiki ya kimataifa kati ya timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 23 na timu ya Taifa ya Shelisheli iliyochezwa jana Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Kaluta jijini Arusha imeingiza sh. 5,014,000.
U23 ilishinda mechi hiyo mabao 3-1. Timu hizo zitarudiana tena kesho (Julai 29 mwaka huu) kwenye uwanja huo huo. Shelisheli iko kwenye ziara ya maandalizi ya michuano ya nchi za visiwa ziliko katika Bahari ya Hindi barani Afrika itakayofanyika mwezi ujao. Visiwa hivyo ni Shelisheli, Mauritius, Comoro, Mayotte, Reunion na Madagascar.
Julai 30 mwaka huu, kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen ambaye yuko Arusha kushuhudia mechi hizo atatangaza kikosi cha Stars ambacho Agosti 7 mwaka huu kitakwenda Palestina kucheza na timu ya Taifa ya nchi hiyo katika mechi itakayofanyika katika kalenda ya FIFA- FIFA dates (Agosti 10 mwaka huu).
Taarifa hii imetolewa na Boniface Wambura, Ofisa Habari wa TFF