MNAJIMU maarufu nchini Tanzania, Sheikh Yahya Hussein (89) amefariki dunia leo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana Dar es Salaam zinaeleza kuwa kifo cha mtabiri huyo kimesababishwa na maradhi ya moyo yaliokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu sasa.
Mtabiri huyo enzi za uhai wake akitabiri mambo anuai jambo ambalo lilimjengea umaarufu, kiasi kwamba iliwahi kuibuka mivutano juu ya utabiri wake.
Taarifa za kufariki kwa Sheikh Yahya zilisambaa kwa muda mfupi jana Jijini Dar es Salaam kuanzia majira ya saa tano asubuhi, baada ya watu kuwasiliana kwa simu juu ya kifo chache.
Akizungumza nyumbani kwa Sheikh Yahya, Magomeni Mwembechai, Dar es Salaam jana, mtoto wa sheikh Yahya, Hassan Yahya alithibitisha kufariki kwa baba yake.
Alisema alfajiri ya jana walizungumza mambo mengi yanayoendelea duniani, lakini saa nne asubuhi hali ya afya yake ikabadilika na kukimbizwa Hospotali ya Mount Ukombozi, Morocco ambapo alifariki majira ya saa tano asubuhi.
“…tutamkumbuka kwa mengi kama watoto wake lakini Watanzania nao watamkumbuka kwa umaarufu wake wa kutabiri mambo mbalimbali yaliyokuwa yanatimia hali iliyomjengea heshima kubwa hata nje ya Tanzania.
…Mwenyezi Mungu amemwita na sote tutakwenda wakati wetu ukifika,”
alisema mtoto huyo wa Sheikh Yahya.
Hassan alieleza kuwa baba yao alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo kwa zaidi ya miaka mitano na aliwahi kupelekwa India kwa matibabu.
Hata hivyo akiwa nchini India kimatibabu, baadhi ya watu waliwahi mvumishia amefariki dunia, jambo ambalo halikuwa kweli.
Akizungumzia taratibu za mazishi, alisema mwili wa Sheikh Yahya aliyefia Hospitali ya Mount Ukombozi, ulitarajiwa kupelekwa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.
“Kwa mujibu wa ratiba …tutamzika mzee wetu katika makaburi ya Tambaza baada ya kufanyika kwa ibada ya sala msikiti wa Tambaza.
… Watakaofika kushiriki shughuli za mazishi wataanza kufika saa nne asubuhi na baada ya hapo ndipo taratibu nyingine zitaendelea,” alisema Hassan.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Sheikh Yahya kutokana na kifo cha mnajimu huyo.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Sheikh Yahya Hussein ambaye enzi za uhai wake alijipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi kutokana na kipaji chake katika masuala ya unajimu wa nyota ambao ulimpatia sifa kubwa,” Rais Kikwete alisema katika salamu zake za rambirambi aliyoitoa.
“Naomba, kama familia, mpokee salamu zangu za pole kwa kuondokewa na kiongozi muhimu na tegemeo kubwa la familia.
“Naelewa fika machungu mliyonayo katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wenu. Najua alikuwa mzazi, alikuwa baba, alikuwa babu, alikuwa mlezi na tegemeo kubwa la familia.