Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Mohammed Ali Mwansasu amesema kuwa Waislamu nchini hawana sababu ya kutoshiriki Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu na kuwa wanaochochea Waislamu wasishiriki Sensa hiyo ni washabiki wa siasa.
Aidha, Sheikh Mwansasu ameipongeza Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kubuni na kutekeleza wazo la shule za sekondari za kata kwa sababu shule hizo ni ukombozi wa watu masikini na familia masikini nchini ambazo hazina uwezo wa kupeleka watoto katika shule binafsi.
Kauli ya Sheikh Mwansasu kuhusu Sensa ni sauti nyingine muhimu katika sauti nyingi za viongozi wa dini ya Kiislamu ambao wamekuwa wanakemea uchochezi wa baadhi ya viongozi wa kikundi kimoja cha Kiislamu ili Waislamu wasishiriki Sensa iliyopangwa kufanyika Agosti 26, mwaka huu, 2012.
Jana, kiongozi mwingine wa Waislamu, Sheikh Khalifa Khamis Khalifa ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Imam Bukhary aliwataka Waislamu kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa na kupuuza propaganda zinazoenezwa na baadhi ya viongozi wa kundi moja la Kiislamu kutaka wasishiriki.
Akizungumza jioni ya jana, Jumapili, Julai 22, 2012, kwenye Futari ya Mfungo wa Ramadhan ambayo Rais Kikwete aliwaandalia wananchi wa Mkoa wa Mbeya wakiwamo viongozi wa dini, Sheikh Mwansasu amesema kuwa dini ni utaratibu wa maisha ambao hauna sababu ya kuwagombanisha Watanzania kwa sababu kila mtu anachagua utaratibu wake wa maisha. Rais Kikwete alikuwa katika ziara ya siku mbili ya Mkoa wa Mbeya.
Sheikh Mwansasu amesema kuwa ni muhimu kwa Waislamu kushiriki Sensa kwa sababu Sensa inalenga kusaidia maandalizi ya mipango ya maendeleo ya nchi. “Serikali itaandaa vipi mipango ya maendeleo ya wananchi bila kujua idadi ya wananchi hao? Hata nyumbani, kila mtu ana sensa yake. Mke wangu nyumbani anatenga na kupakua chakula kila siku kulingana na idadi ya wanafamilia wangu nyumbani – yaani mke wangu, mimi na watoto wetu wawili.”
Kikundi kimoja cha Kiislamu kimekuwa kinawachochea waumini wa dini hiyo wasishiriki Sensa ya Watu na Makazi kama Serikali haikukubali kuongeza swali linalohusu dini za watu katika maswali ya Sensa hiyo. Swali kuhusu dini liliondolewa katika maswali ya Sensa katika Sensa ya kwanza ya Tanzania huru mwaka 1967, miaka 45 iliyopita.
Alisema Sheikh Mwansasu: “Tuache mijadala. Tuache ushabiki wa siasa. Tujiandikishe na kushiriki Sensa. Kwa kushiriki ushabiki wa namna hii ama tunaonyesha kuwa uwezo wetu ni mdogo ama uwezo ni mkubwa lakini tunapindisha mambo makusudi.”
Amesisitiza: “Ndugu zangu Waislamu, hata hapa Mbeya yako maneno haya hata ndani ya misikiti. Vipeperushi vimeandaliwa. Lakini ukweli ni kwamba suala la Sensa siyo la itikadi ya chama. Suala la Sensa ni suala la kitaifa.”
Kuhusu shule za sekondari za kata, Sheikh Mwansasu alisema kuwa shule hizo ni muhimu sana kwa wananchi masikini katika Tanzania na kuwa maneno kuhusu ubora shule linajitokeza kwa sababu shule tayari zipo.
“Sisi masikini katika Tanzania tunashukuru sana kuwa shule hizi zipo. Zimewasaidia sana masikini katika Tanzania. Watoto kutoka familia masikini wangesoma wapi? Hata mwanafalsafa Plato amepata kusema …You cannot talk about quality without first achieving quantity (huwezi kuzungumzia ubora bila kwanza kuwa na wingi),” alisema Sheikh Mwansasu.
Alisema kuwa kauli za baadhi ya watu kuhusu shule hizo na madai kuwa hakuna lolote limefanyika katika Tanzania katika miaka 50 ya Uhuru ni unafiki na uzandiki tu na walionufaika zaidi na matunda ya miaka 50 ndiyo wenye kelele zaidi.